Watakiwa kuheshimu mifumo ya uchaguzi


Margareth Chambiri

MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani amesema jambo kubwa ambalo Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na uchaguzi wa Marekani uliomalizika hivi karibuni ni wananchi kuheshimu mifumo ya uchaguzi.

Mkurugenzi Kailima alitoa kauli hiyo kama tathimi yake kuhusu uchaguzi  wa Marekani na namna baadhi ya watu wanavyohoji ucheleweshaji wa kutangaza matokeo ya uchaguzi unaofanywa na Tume ikilinganishwa na ilivyofanyika Marekani.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM, Kailima alisema si sahihi kulinganisha uchaguzi wa Marekani na Tanzania, akitolea mfano wa sekta ya mawasiliano ambayo ni muhimu katika kusafirisha vifaa na taarifa za uchaguzi inavyokabiliwa na changamoto.

Alisema Watanzania na hasa wapiga kura wengi wanaishi vijijini ambako baadhi ya maeneo hayafikiki kirahisi na haiwezekani Tume ikatangaza matokeo bila kuhakikisha kuwa kila kura imehesabiwa ikiwamo ya mwananchi wa kijijini.

Alibainisha kuwa yapo mambo ya msingi ambayo Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na uchaguzi wa Marekani, kubwa ikiwa ni hatua ya kuheshimu mifumo na mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo.

Alitolea mfano wa uvumilivu katika kusubiri matokeo na wagombea kuheshimu matokeo yanayotangazwa na NEC kwa mujibu wa sheria, kwani hata pale ambapo anayeshindwa hakuridhika, anaweza kupinga matokeo kwa kufuata taratibu za kisheria.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alisema NEC inakamilisha Mwongozo wa Utoaji Elimu ya Mpiga Kura wa 2015/20 ili kushirikisha asasi za kiraia, taasisi au vikundi vya watu wanaotaka kutoa elimu hiyo.

Kwa mujibu wa Kailima, Tume imo katika hatua za mwisho za kupitia Rasimu ya Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya kuupitisha utumiwe na wadau wa uchaguzi.

Alisema pamoja na hatua ya Tume ya kuanza kutoa elimu ya mpiga kura mapema kuliko ilivyozoeleka na wananchi, inakusudia kupanua zaidi wigo wa utoaji elimu hiyo kwa kushirikisha wadau wengi zaidi wakiwamo viongozi wa dini.

Kailima alisema NEC chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Damian Lubuva, baadaye mwezi huu itatoa taarifa rasmi ya kuzialika taasisi na asasi za kiraia zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura, kuwasilisha maombi yao ya kibali rasmi cha kutoa elimu hiyo.

Aidha, Mkurugenzi wa Uchaguzi alitaja vigezo vya kupata kibali cha kutoa elimu, kuwa ni pamoja na cheti cha usajili, asasi au taasisi kufanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kuwasilisha majina ya watendaji wa juu.

NEC imeanza utekelezaji wa utoaji elimu hiyo kwa kushiriki maonesho mbalimbali yakiwamo ya biashara ya kimataifa na ya wakulima na kutembelea na kutoa elimu kwenye shule kadhaa za sekondari nchini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo