Makonda akalia kuti kavu


*Ni kutokana na kauli, uamuzi wake mikutanoni
*Wananchi walalamikia kuzuiwa wauza samaki

Sharifa Marira na Leons Zimbandu

Paul Makonda
SIKU chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutoa kauli ya kujivunia watumishi wanne kati ya 120 na kupiga marufuku uuzaji samaki, mboga mboga na matunda mitaani, wananchi na wanasiasa wamesema kauli za kiongozi huyo hazieleweki wakimtaka azitolee ufafanuzi.

Aidha, wamesema kauli za Makonda zimetoka wakati ambapo Serikali haijajipanga na kwamba haieleweki amelenga nini kiutendaji.

Kauli za wananchi na wanasiasa hao akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Waziri wa Tamisemi zinaweza kutafsiriwa kuwa amekalia kuti kavu, kwa kuwa ndio waangalizi wa shughuli za kila siku za mikoa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, wananchi hao walisema hawaelewi mvutano uliopo kati ya Makonda na watendaji wa ofisi yake unasababishwa na nini, pia hawajui uamuzi wa kuzuia biashara hizo ndogo zinazosaidia wananchi masikini kiuchumi utaisaidiaje jamii.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota alisema katazo hilo limetolewa mapema wakati Serikali haijaweka mipango mizuri kwenye mitaa.

Alisema wafanyabiashara wa mboga mboga au matunda wanaopita mitaani hawajawahi kuwa kero au kuleta adha kiasi cha kusababisha wakatazwe kufanya bishara hiyo na wengi wana mitaji midogo.

‘’Wafanyabiashara wanaopita mitaani, kwanza wengi wana wateja wao tayari ambao wanawapitishia biashara hiyo, wanauza kwa maombi maalumu, lakini pia wana mitaji midogo kama Sh 5,000 au Sh 10,000 mtu huyu ukimtaka aende sokoni kupanga chini biashara yake kwa mtaji upi?’’ Alisema na kuongeza:

“Katazo lilitolewa mapema mno wakati Serikali ikiwa haijajipanga kwa hilo. Kama kuna wanaoona watu hao ni adha, basi ni wachache wanaopita kwenye masuka makubwa kununua mahitaji yao ya ndani, lakini wengi wanawahitaji watu hao wanaoleta biashara majumbani.’’

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Muulizeni mwenyewe, anaweza kutoa ufafanuzi zaidi kama hakueleweka vizuri.’’

Mkazi wa Mbagala Rangi Tatu, Juma Hassan alisema malumbano yanayoendelea baina ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzake, bado  hawajui nini kinaendelea kati yao.

Alisema  watu wanahitaji maendeleo na si vijembe vinavyoendelea kwa kuitana mizigo, kwani  hali ya  ni pasua kichwa hakuna anayependa mipasho.

“Kama kweli wapo wafanyakazi mizigo, basi hatua zichukuliwe, hakuna sababu kila wakati kuzungumza kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Alisema wananchi wanahitaji kusikia ahadi anazotoa zikitekelezwa kwa wakati lakini viongozi wawajibishwe kwenye vikao.

Amanda Sijali mkazi wa Sinza, alisema Mkuu wa Mkoa  anapaswa kuweka wazi hata majina ya watumishi mizigo ili iwe rahisi kwa vyombo vingine kuchukua hatua.

Alisema kitendo cha kuwaamini watumishi wanne mkoa mzima, maana yake wengine watajificha kwenye kivuli hicho, kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Tayari Makonda ametaja viongozi katika ofisi yake kuwa ni mizigo, hivyo Serikali  au wananchi wanafaidika nini kwani hakuna hatua inayochukuliwa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema iwapo Makonda atatambua mipaka yake, atakuwa kiongozi mzuri anayehitaji utendaji kazi.

Alisema kauli zake zinapaswa kuzingatia anazungumzia wapi, walengwa ni kina nani ili kuondoa mkanganyiko ndani ya jamii, lakini hivi sasa anasababisha maswali yasiyo na majibu.

“Makonda ni mtendaji mzuri ambaye anahitaji kuondoa dhana ya  kuongopa kusemana  serikalini kuhusu utendaji,” alisema.

Diwani wa Majohe, Ukonga, Waziri Mwinevyale alisema Mkuu wa Mkoa hawezi kuzungumzia wanasiasa kama yeye, kwa vile si wateuliwa wa Rais.

“Ni wajibu wa Makonda kuzungumzia watendaji walio kwenye ofisi yake  ambao wanaweza ‘kutumbuliwa’, lakini  kwa ngazi za kisiasa hana wajibu huo kisheria,” alisema.
   
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo