Bakwata yapokea ripoti ya awali ya mali


Celina Mathew

Shehe Abubakary Ally
MIEZI mitano baada ya Rais John Magufuli kuagiza viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kuchunguza mali zao, Kamati Maalumu iliyoundwa na Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar bin Zubeir kuhakiki mali hizo, imewasilisha taarifa ya awali ikibainisha changamoto kadhaa.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akikabidhi taarifa ya uhakiki huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,  Shehe Abubakary Ally, alisema wamebaini changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mali kutohakikiwa kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi kama ni za Baraza hilo.

Alibainisha kuwa jambo hilo limesababisha uhakiki huo kutofanyika kwa wakati na kuomba kuongezwa muda, ombi ambao liliridhiwa na Shehe Mkuu.

Julai 6, wakati Rais Magufuli akihutubia Baraza la Eid El Fitr kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, alitaka viongozi wa Bakwata kuhakikisha wanasimamia mali zilizo chini yao ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Kwa agizo hilo, Mufti Zubeir aliunda Tume ya wajumbe wanane kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali ikiwamo misamaha ya kodi iliyoombwa na Bakwata na taasisi zake.

"Leo (jana) tumekabidhi sehemu ya mwanzo ya ripoti ya Tume iliyoundwa na Mufti, kwa kweli tumekumbana na changamoto nyingi kwa kuwa ni kazi kubwa kuhoji, kwa kuwa mali za Bakwata ni nyingi hivyo tumeongezwa muda ili kuikamilisha," alisema Shehe Ally.

Alisema baadhi ya vitu walivyochunguza kwenye ripoti hiyo ni mikataba, viwanja, majengo na mali zingine za Baraza, hivyo baada ya Mufti kuisoma ataeleza kilichojiri kupitia vyombo vya habari.

"Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia kilicho ndani ya ripoti hiyo, maana kiongozi wetu aliyetuagiza bado hajaisoma, hivyo akishaisoma atawaeleza kilichojiri ndani yake," alisema Mwenyekiti huyo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Mufti alisema ameipokea na kutokana na unyeti ulio kwenye kazi hiyo ameamua kuwaongeza muda na kuahidi kuwa ataisoma kisha ataeleza kilichomo.

"Nimepokea ripoti hii, kwa kuwa sijui kilichomo nikimaliza kuisoma nitafanyia kazi mambo yaliyopendekezwa na Tume kwa mujibu wa kilichoandikwa," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo