Watakiwa kufuata waraka kuadhibu kwa viboko


Hussein Ndubikile

Profesa Joyce Ndalichako
WALIMU nchini wametakiwa kutoa adhabu ya viboko kwa kuzingatia waraka na maelekezo ya Serikali ya jinsi ya utoaji adhabu hiyo hususan kwa makosa makubwa yakiwamo ya wizi, uvutaji bangi, kupigana na kuharibu mali za shule.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kwenye ufunguzi wa mdahalo wa kujenga na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

Alisema kwa mujibu wa waraka huo, walimu na viongozi wa shule wanatakiwa kuweka bayana makosa na hatua za kinidhamu zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wanafunzi wanaobainika kuvunja sheria.

“Naomba nichukue fursa hii kuielewesha jamii, kuwa sheria hizi zimetungwa kuadabisha wanafunzi ili wawe kwenye mstari sahihi utakaowasaidia kujifunza si vinginevyo,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, wazazi na walimu wanatakiwa kushirikiana kutimiza azma iliyokusudiwa ya kumpa mwanafunzi elimu na stadi bora itayojenga misingi ya maadili inayokubalika kwenye jamii.

Alisisitiza kuwa Serikali imebaini kuwapo malalamiko kwa baadhi ya walimu na bodi za shule zimekuwa zikipelekewa wanafunzi wakorofi na  zinawatetea bila kuchukua hatua stahiki hali inayowapa kiburi na kuamua kuwafanyia vitendo viovu.

Aliagiza kuacha kuingiza siasa kwenye usimamizi wa maadili huku akitaka wahusika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maelekezo yanayotolewa.

Aliasa wanafunzi kuepuka kuwa wahanga wa teknolojia inayochochea kwa kiasi kikubwa chanzo cha kuwabadili mienendo na misingi ya maadili yakiwamo matumizi ya mitandao ya kijamii.

Pia aliwaasa kuacha kuangalia masuala yasiyofaa kwenye mitandao hiyo badala yake waitumie kujifunzia masomo yao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo