‘Scorpion’ asomewa maelezo ya awali


Jemah Makamba

MSHITAKIWA wa kesi ya wizi na kujeruhi kwa kutoboa mtu macho, Salim Njwete ‘Scorpion’ amefikishwa mahakamani kusomewa maelezo ya awali (PH) ambapo katika mashitaka  yake  alikana kutoboa macho na kuiba lakini akakiri kuwa mwalimu wa karate na kukana kuitwa Scorpion.

Alifikishwa mahakamani hapo jana saa mbili asubuhi akiwa kwenye gari dogo la Polisi akiwa peke yake na pingu mikononi. 

Mshitakiwa alifikishwa kwenye chumba cha Mahakama ambapo kesi yake iko mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule ambaye alimpaMwendesha Mashitaka, Nassoro Katuga karatasi yenye malalamiko kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo hayo.

Katuga alimsomea jina lake na kumwuliza kama ni kweli anaitwa hivyo au sivyo na mshitakiwa kusema anaitwa Salim Njwete na kukataa jina la Scorpion akisema halitambui.

Aliulizwa kama yeye ni mwalimu wa karate na kama alipata mafunzo ya mchezo huo kati ya mwaka 1989 na 1995 Ifakara, Morogoro akajibu kuwa ni kweli.

Katuga alimwuliza kama aliwahi kuwa mlinzi wa baa ya Kimboka, Buguruni, akakana.

Alipoulizwa kuhusu kuhusika na wizi kwa kutumia kisu na kumjeruhi malalamikaji tumboni, mabegani na kumtoboa macho, pia alikana.  

Aliulizwa baada ya tukio hilo alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi, Buguruni ambako alikiri kwa maandishi kuhusika, alikana pia.

Mwendesha Mashitaka alisema kutokana na kifungu cha sheria cha 234 sura ya 16 kuruhusu mshitakiwa kutenganishiwa mashitaka, katika mashitaka yanayomkabili alitenganishiwa mashitaka ya wizi na ya kujeruhi, hivyo kuwa na kesi mbili.

Upande wa Jamhuri ulimwomba Hakimu awapangie tarehe ya karibu ili usikilizaji kesi uanze ambapo ulisema unatarajia kuwa na mashahidi sita.

Hakimu alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa Desemba 14 na mshitakiwa ataendelea kukaa mahabusu hadi siku hiyo.

Njwete alikamatwa kwa tuhuma za kumwibia Saidi Mrisho vitu na fedha vya thamani ya Sh 476,000 na kabla na baada ya kumwibia, alimjeruhi kwa kumchoma kisu tumboni, mabegani na kumtoboa macho, Buguruni Sheli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo