Mabadiliko na maendeleo yanahitaji ubabe—Waziri


Dotto Mwaibale


George Simbachawene
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, amesema ili kusimamia mabadiliko na kuleta maendeleo ya nchi na maadili, kunahitajika kiongozi mbabe na mtemi.

Simbachawene alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya uongozi na maadili kwa wahitimu 47 wazalendo kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, baada ya kumaliza ujenzi wa kujitolea kwa mwezi mmoja Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema ili kusimamia mabadiliko na maendeleo, nchi inatakiwa kuwa na mtu mbabe na mtemi na si kutegemea kundi fulani la watu, kwani kufanya hivyo, kila kundi litahitaji kupendelewa baada ya kujiona bora kuliko lingine.

Alisema bila kuwa na viongozi wenye maadili, nchi haiwezi kusonga mbele kwani tangu kuachwa mfumo wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambako kulitolewa mafunzo ya maadili, athari zake zilijitokeza.

Akifafanua athari hizo, Simbachawene alisema ndipo kwa kipindi cha miaka 20 CCM ilivamiwa na matajiri wakitaka nafasi za uongozi wa ngazi za ubunge, urais na ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama.

"Napenda kusema kuwa tunahitaji mabadiliko makubwa ya kufumua chama chetu hasa katika mfumo mzima wa kupata viongozi, kwani uliopo umetufanya tupoteze baadhi ya nafasi katika majimbo na hata kwenye uchaguzi mdogo.

“Kutokana na mfumo mbaya tulishindwa baada ya wanachama wetu kumpigia kura mtu mwingine kwa hasira, huku vikao vyote vikiendeshwa kwa misingi ya fedha," alisema Simbachawene.

Alisema ilifika hatua kila jambo lilikuwa haliwezi kufanyika bila kuomba ufadhili kwa matajiri ambao wengi wao ndio walikuwa wakwepa kodi.

Aliongeza kuwa watumishi wa umma wamekuwa wakilalamika kuwa hali ya maisha ni ngumu huku wengine wakisema Hazina hakuna fedha, wakati hakuna hata mwezi ambao mtumishi amekosa mshahara.

Alisema pengine hali hiyo inatokea kwa kuwa watumishi hao walikuwa wakitegemea kitu kingine mbali ya mshahara, baada ya mianya hiyo kufungwa,   wanalalamika.

Aliongeza kuwa awali bandarini kulikuwa na pilikapilika nyingi za mlundikano wa kontena na magari, lakini makusanyo yalikuwa hayafiki hata Sh bilioni moja kwa mwezi, lakini sasa pilikapilika hazipo zinakusanywa Sh trilioni moja “hii inaonesha kodi ilikuwa hailipwi ipasavyo”.

Alisema nchi ilifikia pabaya, kwani kila sehemu kulikuwa na madalali iwe hospitali, ofisi za Serikali, mahakamani na hata kwenye kupata vyeo  lakini hivi sasa mianya hiyo imezibwa.

Alisema anachokifanya Rais John Magufuli ni mabadiliko ili watu waache kuishi kwa mazoea na nchi ipige hatua katika masuala yote.

Simbachawene alisema changamoto kubwa iliyopo ni kuchanganya sera za siasa na za uongozi, jambo linalosababisha mambo mengine kushindwa kusonga mbele.

Mkuu wa Chuo, Profesa Shadrack Mwakalila alisema baada ya kuona mmomonyoko wa maadili miongoni mwa Watanzania hasa kwa baadhi ya viongozi, chuo kimeona ni vema kurejesha mafunzo ya uongozi na maadili ili kupunguza kama si kumaliza kasi ya mmomonyoko wa maadili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo