Mbunge asikitishwa wanayama kuuawa

Joyce Kasiki, Dodoma

MWENYEKITI wa kupambana na ujangili bungeni, Riziki Lulida, amesikitishwa na kasi ya kuuawa kwa wanyamapori kwenye hifadhi  nchini wakiwamo tembo na simba.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana,  Riziki  alisema iwapo kasi hiyo itaendelea, miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa haina tembo hata mmoja na kuifananisha na Ivory Coast.

Riziki ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Lindi kupitia   CUF, alisema kuuawa kwa wanyama hao kunasababishwa na wawindaji haramu kuwinda katika maeneo ya mapito ya wanyama lakini pia wafanyabiashara kuachwa muda mrefu wakiwinda kwenye hifadhi hizo.

"Ivory Coast, Rwanda na Burundi zilijulikana huko nyuma kuwa na tembo wengi lakini hivi sasa, hazina tembo huku akisema waliobaki Tanzania wanaelekea kumalizwa, kwani kasi ya kuwaua ni kubwa,” alisema na kuongeza:

“Tanzania tuna Niassa Selous Corridor, ambayo ilikuwa ikipitishia tembo kama ilivyo ya Serengeti Masai Mara ya kupitishia nyumbu na pundamilia na wanyama wengine, lakini ile ushoroba wa Niassa tangu nchi ipate uhuru, haujawahi kutangazwa.”

Hata hivyo, alisema lazima Serikali kwa kushirikiana na Bunge na wananchi  wasimamie kidedea,  kuhakikisha wanatoa sauti ili kuhakikisha tembo wanalindwa ipasavyo kwa manufaa ya Taifa na vizazi vijavyo.

Riziki alisema Tanzania inaonekana imeacha utalii endelevu wa kuangalia ushoroba wa tembo kutoka Selous kwani hautangazwi ambapo matokeo yake miti imekuwa ikikatwa na kuondoa uhalisia wa awali.

“Kwa nini wa Serengeti unatangazwa halafu zingine kama vile Niassa hazitangazwi, huku shoroba za wanyama zimekuwa zikionekana kuharibiwa maana hazina hata miti,tunatakiwa kuheshimu tulivyonavyo,” alisisitiza Mbunge huyo.

Kuhusu kuuawa kwa samba, alisema mnyama huyo ni miongoni mwa wanaopotea kwa kasi kutokana na uwindaji haramu.

Alisema hivi sasa ni tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo simba walionekana hadharani tofauti na kwenye hifadhi.

"Zamani ilikuwa ukipita njiani kwenye Kipiri kidogo tu lazima ukutane na simba, lakini sasa hivi hawapo na hata ukipita kwenye hifadhi ,bado kumwona simba ni shida," alisema. 

Mbunge huyo aliitaka Serikali kuweka ulinzi wa kutosha kwenye hifadhi ili kuhakikisha wanyama wote wanalindwa kikamilifu ili kukuza vivutio vya utalii na kuvifanya kuwa endelevu na kuliingizia Taifa pato la kutosha.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo