Yanayompata Maalim yatampata Lipumba


Sharifa Marira

Magdalena Sakaya
YALIYOMKUTA Katibu Mkuu wa CUF mkoani Mtwara  ya kukwama kwa mikutano yake ndiyo yatakayomkuta Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, atakapokwenda Zanzibar.

Mkutano wa Maalim Seif uliokuwa na lengo la kukagua shughuli za chama, kupata maoni na mapendekezo kuhusu namna ya kuboresha utendaji wa chama ngazi ya chini, ulipangwa kufanyika Novemba 19   kwenye Chuo cha Stella Maris, Mtwara ulizuiwa na Jeshi la Polisi.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bara, Magdalena Sakaya alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kukwama kwa ziara ya Maalim Seif, Mtwara, akidai kwamba hapana sababu ya kusaka mchawi kwa kuwa hawakufuata taratibu.

Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, alisema ni vigumu Profesa Lipumba kwenda Zanzibar kufanya mikutano ya kuimarisha chama, kwani anatakiwa awasiliane na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar,Nassor Mazrui, ili amwandalie mikutano jambo ambalo haliwezekani bila kupatana viongozi hyao wawili wanaokinzana.

‘’Kilimchomkuta Maalim Seif alistahili na kamwe asitafute mchawi kwani mikutano ambayo alitaka kuifanya hakufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kunipa taarifa mimi, ili niwasiliane na makatibu wa wilaya waandae mikutano yao na polisi walikuwa sahihi kuuzuia kwani kungetokea fujo,’’ alisema Sakaya na kuongeza:

‘’Hata leo mimi au Profesa Lipumba tukitaka kwenda Zanzibar lazima tuwasiliane na Mazrui hatuwezi kufika moja kwa moja, tunaweza kukwama, hatima ya mikutano yetu kule iko mikononi mwa Maalim Seif na Mazrui.’’

Alisema kinachotakiwa kufanyika ni viongozi hao wawili, Maalim Seif na Profesa Lipumba kukubali kukaa meza moja kumaliza tofauti zao na kunusuru chama.

“Maalim Seif anakubalika Zanzibar, Lipumba Bara, hatima ya CUF ni lazima viongozi wakae chini hakuna njia nyingine, kinachoumia ni chama, tusiweke mbele kushinda na kushindwa,’’ alisema Sakaya.

Alisema watu wamezoea kuzusha maneno, kwamba polisi wanaruhusu mikutano ya Lipumba na kuzuia ya Maalim Seif, lakini kilichotokea Mtwara kilikuwa sahihi kwani taratibu za kuomba mikutano hazikufuatwa.

“Polisi waliona kuruhusiwa kwa mkutano huo lolote lingeweza kutokea kwani waliokwenda kuomba kibali hawakufuata utaratibu na si viongozi bali wanachama wa kawaida, ambao hawana nafasi ya kuomba kibali chochote, ndiyo maana polisi walitutaka kama chama tukae tuelewane  ndipo tuombe kibali,” alisema.

Alisema kilichotokea Mtwara ni sehemu tu ya kinachoweza kutokea maeneo mengine Bara, endapo Maalim Seif ataendelea na utaratibu wa kukiuka Katiba na taratibu halali za chama na kwamba yuko tayari kumwandalia mikutano, ila isiwe ya kunadi chuki au kumkataa Profesa Lipumba.

Sakaya aliwahadharisha wanasiasa wanaoingilia mgogoro huo kwa lengo la kubomoa chama kwamba wakae mbali, hawahitaji msaada wa kichochezi.

“Kuna wanasiasa wanataka kutumia mgogoro huu kuendeleza vyama vyao, wakae chonjo, hakuna chama ambacho hakijapata kukumbwa na migogoro, lakini CUF hatujawahi kuviingilia kwa nia ya kuvibomoa wala kujinadi kwa ajili ya chama kingine,” alionya Sakaya.



Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo