Mwenyekiti wa kijiji adaiwa kuuza ardhi kinyemela


Moses Ngwat, Mbarali

MWENYEKITI wa Kijiji cha Nyeregete, wilayani Mbarali, Moses Fute, anatuhumiwa kuuza ardhi inayomilikiwa na kijiji hicho kwa watu binafsi, wakiwemo viongozi wa Serikali, askari polisi na mahakimu, huku mwenyewe akijimilikisha ekari 300.

Ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 2671.4 ilitengwa na kijiji hicho kwa ajili ya mradi wa kuwaendeleza vijana katika kilimo cha mpunga kwa kuwagawia ekari tano kwa kila kijana ambaye alihitaji kujihusisha na shughuli za kilimo.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Ruben Mfune ameagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya mwenyekiti huyo na wote waliohusika na uporaji huo wa ardhi kwa kuwa ndio wamekuwa chanzo cha migogoro katika wilaya hiyo.

Akiwahutubia wananchi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara juzi, mkuu huyo wa Wilaya ya Mbarali alitoa siku 14 kwa wataalamu wa ardhi wilayani humo na viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa kupima upya eneo hilo na kuligawa kwa wananchi.

“Nimeagiza hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika na hujuma hizi, lakini pia nimeagiza hadi kufikia tarehe 10 mwezi ujao (Disemba) viongozi wa mamlaka na wataalamu wa ardhi wawe wamemaliza kupitia upya mchakato wa ugawaji ili kila mwananchi apate ardhi ya kilimo” alisema Mfune.

Kadhalika, mkuu huyo wa wilaya amewataka wale wote waliouziwa mashamba na kuanza shughuli za kilimo katika eneo hilo kusitisha mara moja na kwamba atakayekutwa akijihusisha na shughuli yeyote katika eneo hilo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Awali, akielezea sakata hilo Kaimu Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji wa Rujewa, Fortnatus Mjengwa, alisema sakata hilo la kuuzwa kwa aridhi ya  kijiji lilitokea kabla ya kijiji hicho kuvunjwa na kujumuishwa kwenye eneo la Mamlaka ya Mji mdogo wa Rudewa.

Hata hivyo, Mjengwa alisema kuwa ardhi hiyo iliyouzwa ilihusisha vitongoji vinne na kwamba tayari wamemaliza kuhakiki na kuyapima maeneo yote yaliyouzwa katika vitongoji hivyo na  pindi mchakato wa kuorodhesha majina ya wanakijiji wote wenye uhitaji wa mashamba ukikamilika watayagawa.

Akifafanua zaidi alisema baada ya kupima upya ilibainika kuwa kitongoji cha Maborishi kina ekari 1121 zilizouzwa, kitongoji cha Mangenyu ekari 390 ambazo zilitengwa kwa ajili ya wafugaji, Katenge ekari 337 na Kitongoji cha Nyamto ekari 823 ambazo nyaraka za waliouziwa zinaonyesha vigogo mbalimbali wa serikali.

“Kuna watu wameuziana ekari 500 wakati sheria ya ardhi iko wazi juu ya nani ana mamlaka ya kuuza eneo kubwa kama hilo. Kibaya zaidi walionunua wapo waheshimiwa mahakimu, watendaji wa halmashauri, hadi viongozi wa polisi na ndio maana kila wananchi walipojaribu kulalamika mwisho wake ilikuwa ni kukamatwa na kuwekwa ndani” alifafanua Mjengwa.

Hali hiyo ya kurudishwa mikononi mwa kijiji na kuamuliwa kugaiwa kwa wananchi ilipokerewa kwa furaha kubwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo na kumuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuendelea na hatua hiyo katika maeneo mengine yenye migogoro.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo