Lwakatare alalamikia ugawaji misaada kwa waathirika wa tetemeko


Abraham Ntambara

Wilfred Lwakatare
WAZIRI Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare, amesema hakuridhishwa na utaratibu uliotumiwa na Serikali kushughulikia suala la waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Kinachomkera ni kuelekeza michango yote kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Akazungumza juzi kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV, Lwakatare alisema Serikali ilitakiwa kuainisha misaada iliyostahili kupitia kwa Mkuu wa Mkoa na ambayo ingepelekwa moja kwa moja kwa wananchi.

“Mimi niliguswa na tatizo hili na pia nilikuwa wa kwanza kuutilia shaka utaratibu huo. Kweli awali Serikali ilikuwa na nia njema, lakini ilitakiwa iache mianya mingine ya kusaidia wahanga,” alisema Lwakatare.

Alisema Serikali ilitakiwa kuwa na mtazamo wa mbali kwanza wa kuangalia sehemu iliyoathirika ambao ni wananchi badala ya kwenda moja kwa moja kwa Mkuu wa Mkoa.

Alisema katika kushughulikia suala hilo, alitoa ushirikiano mkubwa kwa Mkuu wa Mkoa na kubainisha kuwa  baada ya Serikali kutoa masharti magumu kwa wahanga hao kwamba waanze kujihudumia, aligawa maturubai na mablanketi kwa wahanga.

Mbunge huyo alisema pia alitafuta wadau wakiwamo wabunge ili wasaidie  kutoa misaada ya kuhudumia wananchi wa Kagera na kwa kuona kuwa kama angechangisha fedha, kungeleta shida, alitafuta mfanyabiashara wa kusambaza huduma.

Alisema wadau ambao aliwatafuta alitaka wafike kwa mfanyabiashara huyo na kulipia fedha za vitu ambavyo wangependa kuvitoa kama mchango, ili mfanyabiashara huyo avichukue na kuvisambaza kwa waathirika.

Alifafanua kuwa utaratibu huo ulikumbwa na vikwazo kutokana na kwamba Jeshi la Polisi Kagera lilikamata mfanyabiashara huyo kwa kutoa huduma hiyo, lakini Lwakatare baada ya kwenda kutoa ufafanuzi, aliachwa kwani alionekana hana tatizo na kuendelea kutoa huduma hadi mzigo ulipokwisha.

Akizungumzia migogoro ya ardhi inayoendelea nchini kwa nafasi yake ya Waziri Kivuli, alisema tatizo kubwa ni mfumo ambao haukuainisha maeneo kulingana na matumizi.

Lwakatare alimpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kwa juhudi ambazo amekuwa akifanya kutatua migogoro na kwamba amepiga hatua nzuri baada ya kufanya upimaji wa ardhi katika mkoa wa Morogoro.

Aidha, alimtaka Waziri huyo hata kama bajeti aliyopewa ni ndogo, lakini ahakikishe anaiwekeza katika upimaji huo wa ardhi ili kupata suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo la ardhi nchini.

Alisema kama yeye angekuwa Waziri kamili angehakikisha kila senti anayopata kwenye Wizara hiyo anaielekeza kupima ardhi kwa kuwa ndilo ambalo litafanya kuondokana na migogoro ya ardhi nchini.

Lwakatare aliishauri Serikali kushughulikia waliosababisha kwa makusudi   migogoro kwa kupokea rushwa na kugawa ardhi zaidi ya mara moja na kwa kuwa wana mali basi zitaifishwe.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo