Mahakama yashangaa Lissu kutokamatwa


Grace Gurisha

Tundu Lissu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshangazwa na upande wa mashitaka kushindwa kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) licha ya kutoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo, na kusema uliogopa kutekeleza agizo hilo halali.

Mahakama hiyo imeweka bayana kuwa haimwogopi Lissu, wala haina mpango wa kupambana naye, bali Mbunge huyo anachotakiwa ni kufuata mfumo wa sheria uliopo na kwa hadhi yake hatakiwi kufanya vitendo anavyofanya sasa dhidi ya Mahakama kwa sababu yeye ni kioo cha jamii.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba alifikia hatua hiyo jana, baada ya Lissu kuvunja masharti ya dhamana mara mbili mfululizo katika kesi ya uchochezi inayomkabili yeye na wenzake watatu, akiwamo Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina.

Simba alimhoji Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Mwita: “Amri ya kumkamata Lissu ilitolewa na wewe ulisaini hati hiyo, iweje hakukamatwa hadi leo (jana) na wakili wake, Peter Kibatala anadai kuwa mteja wake amekuja mwenyewe mahakamani wakati ilitakiwa aje chini ya ulinzi?”

Aliongeza: “Wewe kama wakili ulifanya jukumu gani la kuhakikisha Lissu anakamatwa? Kwa nini hamkumkamata, hamwoni kama mnaidharau Mahakama au mnamwogopa? …Haiwezekani Mahakama inatoa hati nyie hamuitekelezi.

“Si kwamba nataka kupambana na wewe (Lissu), hapana bali kutokana na nafasi yako, haifai kufanya mambo kama haya. Nakwambia hatukuogopi, tutaogopana katika mambo mengine, lakini si katika suala la kufuata sheria na wewe ni mwanasheria unajua taratibu zote.

“Tunafanya hivi ili jamii ione, kwa sababu haiwezekani watu wengine wanafuata utaratibu halafu wengine hawafuati, hilo halitawezekana,” alisema Simba.

Akijibu hoja za Hakimu Simba, Wakili Mwita alisema alipeleka hati hiyo katika kituo cha Polisi husika, hivyo hana jukumu la kumkamata.

“Lakini naomba radhi kwa kutokamatwa kwa mshitakiwa huyo na ninaiachia Mahakama  jukumu  la kufuta dhamana,” alisema Mwita.

Hata hivyo, hakimu huyo alisikitika kutumia muda mwingi kulumbana na mambo anayoyasababisha Lissu, akisema muda aliopoteza angeweza kusikiliza shahidi hata mmoja na kumtaka Mbunge huyo kujirekebisha.

Lissu alipopewa nafasi ya kujieleza kwa nini hakuonekana mahakamani mara mbili mfululizo bila taarifa, alidai kuwa alipata safari ya ghafla kwenda Ujerumani na mara ya pili alishindwa kufika kwa sababu alikwenda Mwanza kwenye kesi ya uchaguzi, ambayo ilitakiwa kwisha ndani ya muda na safari zote hizo aliipa taarifa Mahakama kwa maandishi.

Hakimu Simba alipinga sababu hizo na kusema bado alikuwa na nafasi ya kuandika barua na aliyodai kuandika haipo mahakamani.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 20 itakapotajwa huku Hakimu Simba akiamuru dhamana za washitakiwa kuendelea kwa sababu upande wa mashitaka uliogopa kumkamata Lissu.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni Mmiliki wa Mawio Mkina, Mhariri Jabir Idrisa na Mchapaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Ilidaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, Dar es Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho: ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo