Chadema yabuni njia mpya ya mapato


Peter Kimath, Mlimba

Freeman Mbowe
CHADEMA imetangaza mpango wa kuacha kutegemea ruzuku ya vyama vya siasa kutoka Serikali Kuu kwa kuanza kutoa kadi za uanachama kwa mfumo wa elektroniki utakaoiingizia mapato makubwa.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alibainisha hayo juzi kwenye mkutano na watendaji wa chama hicho jimboni Mlimba, wilayani Kilombero ukihusisha viongozi wa chama hicho ngazi za vitongoji, vijiji, kata na wabunge.

Alisema ifikapo mwakani, chama kitaanza rasmi kutumia kadi za elektroniki kwa wanachama wake badala ya zile za zamani kwa lengo la kutumia kadi hizo kama chanzo kikuu cha mapato.

 "Tutakapoanza kutumia mfumo huo wa kadi za elektroniki utawezesha wanachama kunufaika na mapato yatakayotokana na uuzaji wa kadi hizo badala ya kutegemea ruzuku pekee kuendesha chama,’’ alisema Mbowe.

Alisema fedha zitakazokusanywa kutokana na mauzo hayo hazitakwenda Taifa na badala yake zitakwenda ngazi husika hususan kwenye majimbo ili kutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwamo kujenga ofisi za chama, vifaa vya uenezi na masuala mengine.

Mbunge wa Mlimba ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa, Suzan Kiwanga alisema kumekuwa na kuzorota kwa ununuzi wa kulipia ada za uanachama na hivyo chama kukosa mapato na kutaka wanachama kuchangamkia kununua kadi hizo mpya pindi mchakato utakapokamilika.

Kiwanga alisema uongozi wa CHADEMA umebadilisha mfumo wa utoaji kadi kwa kuweka progamu maalumu ya kutambua wanachama wake nchi nzima kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Mkazi wa Mlimba, Renatus Shija, alisema kukamilika kwa mfumo huo kutawezesha wanachama kuwa na kadi za uhakika ambazo zitawawezesha kutambulika na kuuomba uongozi wa kitaifa kuwajengea uwezo kwa kufanya vikao vya ndani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo