Shauri la Samaki wa Magufuli laibuka


Grace Gurisha

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Desemba 7 inatarajia kutoa uamuzi wa maombi ya upande wa utetezi katika kesi ya kuvua samaki bila kibali, maarufu kama ‘Samaki wa Magufuli’ ya kutaka warudishiwe meli ya Tawaqar I, tani 296.3 za samaki na Sh bilioni 2.

Kesi hiyo, ilikuwa ikiwakabili raia wawili wa China, Hsu Tai na Zhao Hanquing ya kuvua samaki kwenye bahari ya Hindi bila kibali.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na mawakili Kapteni Bendera na John Mapinduzi, ambao wanadai mmiliki wa mali hizo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Al Araim Sea Tawaqar LLC Oman, Said Ali Mohamed.

Mawakili hao walifikia uamuzi huo, baada ya raia hao kushinda rufaa waliyokata kupinga adhabu ya kifungo jela.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga aliwasilisha pingamizi la awali akiiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu yana upungufu kisheria.

Wakili wa Serikali Mkuu,Timony Vitalis alieleza mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi kuwa anapinga maombi hayo kwa sababu tayari kesi hiyo ilikwishatolewa hukumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ikiamuru Serikali kulipa meli ya uvuvi na samaki waliokamatwa miaka mitano iliyopita.

Alidai kwamba inashangaza kuona upande wa utetezi unamtaja Mohamed kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli hiyo na kwamba haijampa mali zake, wakati si mmiliki.

Vitalis aliendelea kudai kuwa hukumu ya Kisutu ilishafutwa na Mahakama ya Rufani ambayo iliwaachia huru baada ya kushinda rufani yao, hivyo Mahakama Kuu haina mamlaka tena ya kujiwezesha kumjua mmiliki halali.

“Kama kesi ilishafutika na vielelezo vikarudishwa kwa wahusika, utaiombaje Mahakama imtambue mmiliki wa mali hizo?” Alihoji.

Pia alibainisha kwamba meli hiyo haiko mikononi mwa Mahakama hiyo, hivyo kwa sasa haina mali hizo kutokana na hukumu kutolewa.

Kutokana na mvutano wa kisheria na hoja, Jaji Munisi aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 7 atakapotoa uamuzi.

Februari 23, 2012 Mahakama Kuu iliwahukumu Hsu na Zhao kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuwatia hatiani kwa kufanya uvuvi haramu.

Machi 28 mwaka huu, Mahakama ya Rufani iliwaachia huru baada ya kushinda rufani yao ya kupinga adhabu ya kifungo hicho au kulipa faini ya Sh bilioni 20 iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo