Temesa yaidai Tanesco


Mwandishi Wetu, Kigoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) linadaiwa kiasi cha Sh. milioni 41 na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Kigoma, ikiwa ni malimbikizo ya madeni kutokana na matengenezo ya magari mbalimbali yaliyofanywa na shirika hilo mkoani humo.

Meneja wa Temesa, Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Hassan Karonda alitoa madai hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Temesa, Dk. Mussa Mgwatu alipotembelea kituoni hapo.

Meneja huyo ameeleza kuwa kwa sasa Temesa Kigoma ipo katika operesheni ya kukusanya madeni kutoka kwa taasisi na kampuni inazozidai.

“Mtendaji  Mkuu tunazidai Taasisi mbalimbali kiwemo Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, Sh. million 41 hadi sasa,” alisema Mhandisi Karonda.

Hata hivyo Dk. Mgwatu alimtaka Mhandisi Karonda kuhakikisha kuwa anakusanya madeni yote anayodai  mkoani humo haraka iwezekanavyo.

 “ Fuatilia ofisi kwa ofisi kukusanya madeni ili kukiwezesha kituo hiki kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa,” alisisitiza Dk. Mgwatu.

Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo Dkt. Mgwatu pia alipata fursa ya kutembelea  kivuko cha MV. Malagarasi na kuona utendaji kazi wake.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Temesa, Dk. Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kutembelea vituo vya wakala hiyo nchi nzima kujionea utendaji kazi wa vituo hivyo. 

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo