Waziri aonya vituo vya chanjo


Hussein Ndubikile

Ummy Mwalimu
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa onyo kwa vituo vinavyotoa chanjo ya homa ya manjano bila vibali kuacha mara moja kabla havijachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, imewahadharisha watu wanaochapisha, kusambaza na kuuza vyeti vya chanjo hiyo, kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kuwapo vituo visivyo na vibali vinavyotoa chanjo ya ugonjwa bila ruhusa ya wizara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa vyeti na mihuri mipya ya chanjo ya ugonjwa huo, Waziri  alisema wizara imeshapata taarifa ya vituo vinavyoendesha huduma hiyo bila vibali, hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu na sheria za utoaji chanjo hiyo.

“Wizara inatoa onyo kwa vituo vinavyoendelea kutoa chanjo bila vibali viache  na wale wanaovichapisha na kuvisambaza waache, tutawachukulia hatua kali kisheria,” alisema.

Alisema tangu ugonjwa huo uripotiwe Desemba mwaka jana iliripotiwa kuwa idadi ya wagonjwa wa homa hiyo nchini Angola ni takribani watu 4,347  huku 377 wakiripotiwa kupoteza maisha na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wagonjwa walikuwa 2,987  waliofariki dunia ni 121.

Alisisitiza kuwa makundi ambayo yamo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo ni wasafiri, watu wanaojihusisha na shughuli za kitalii na uwindaji pamoja na wafanyakazi wa viwanja vya ndege.

Aliongeza kuwa gharama za huduma za chanjo ya homa ya manjano ni Sh 20,000 kwa raia za watanzania na dola 50 kwa raia wa kigeni.

Waziri Ummy alisema chanjo hiyo itatolewa katika vilivyoko viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza, Bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Kigoma na Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja.

Vingine ni mipakani Horohoro, Namanga, Holili, Tarakea, Sirari, Isaka, Mutukula, Mtambaswala, Kasumulu na Tunduma.

Pia alisema utoaji chanjo hiyo unakabiliwa na changamoto ya kuwapo  baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu maarufu kama vishoka ambao hughushi vyeti vya chanjo na kuwapa wasafiri pasipo kuchanja.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi alisema ugonjwa huo bado haujaingia nchini, tangu ulipotokea mwaka 1960 huku akiongeza upo nchi jirani za Kenya, DR-Congo na Angola.

Katika hatua nyingine, Serikali imesajili waganga wa tiba asili na tiba mbadala 14,000 na vituo vya 180.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo