Mbatia alazwa hospitalini India


Fidelis Butahe

MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amelazwa katika hospitali ya Zydus, India tangu Novemba 11 akisumbuliwa na maradhi ya mguu.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa Mbatia alipelekwa nchini humo baada ya kupata maumivu makali ya mguu, huku matibabu aliyopewa nchini yakielezwa kutompa nafuu.

Msaidizi wa Mwenyekiti mwenza huyo wa Ukawa, Hamis Athuman alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kulazwa kwa kiongozi huyo na kutaka taarifa zaidi waulizwe viongozi wa chama na Bunge kwa kuwa yeye si msemaji.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alithibitisha kulazwa kwa Mbunge huyo na kuieleza JAMBO LEO kuwa  anaendelea vizuri na atarejea nchini siku yoyote kuanzia leo.

“Kwa sasa hali yake imeimarika na anaweza kurejea nchini muda wowote,” alisema Owen muda mfupi baada ya kutaka apewe muda ili kuuliza kiundani maendeleo ya afya ya Mbunge huyo.

Habari zaidi kutoka ndani ya chama hicho zilieleza kuwa Mbatia aliondoka nchini Novemba 10, baada ya kufika nchini humo alilazwa.

“Novemba 14 alifanyiwa upasuaji wa mguu, kwa sasa anaendelea vizuri ingawa bado hajaruhusiwa kutoka hosptalini,” zilieleza habari hizo.

Zilifafanua kuwa kwa muda mrefu kiongozi huyo amekuwa akisumbuliwa na mguu na kupewa matibabu maeneo mbalimbali bila mafanikio.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Danda Juju alisema Mwenyekiti huyo amepata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji na kufafanua kuwa huenda akarejea nchini mwishoni mwa wiki hii kutokana na afya yake kuimarika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo