Wakili aomba Kitilya aachwe huru


Grace Gurisha

WAKILI Alex Mgongolwa ameiomba Serikali imwache huru aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya kwa madai kuwa waliomshitaki wameshindwa kukamilisha upelelezi wa kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi.

Katika ombi hilo alilolitoa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipotajwa, Wakili huyo alipendekeza baada ya Kitilya kuachwa, upelelezi uendelee na utakapokamilika, mteja wake aliyedai kuwa anateseka gerezani kwa miezi minane sasa akamatwe tena.

“Tunaomba Mahakama iweke ukomo katika upelelezi au upande wa mashitaka ufute kesi hii na watakapomaliza upelelezi wamkamate tena, kwa sababu tangu mwaka jana wanachunguzwa. Mtu akifikishwa mahakamani lazima hatima yake ijulikane mapema.

“Mwelekeo wa Jamhuri ni kupoteza mwenendo wa kesi wa Mahakama, kwa sababu kila siku wanakuja na wimbo wa upelelezi bado, huu wimbo ni hatari na hauna ukomo,” alidai Mgongolwa.

Alitoa malalamiko hayo baada ya Wakili wa Serikali, Elia Athanas kuieleza Mahakama kuwa upelelezi bado na timu ya uchunguzi wa kesi hiyo bado inaendelea nan upelelezi.

Hata hivyo, Hakimu Mkeha alisema jalada linapokosa mtu maalumu linaweza kupoteza mwelekeo, upande wa Jamhuri unatakiwa kuweka mtu maalumu atakayeulizwa na kujibu, tofauti na ilivyo sasa kwenye kesi hiyo. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 2.

Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine ni aliyekuwa Mrembo wa Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na aliyekuwa mgombea ubunge wa Arumeru Mashariki, Sioi Solomon wote wakiwa wafanyakazi wa benki ya Standard Chartered.

Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo, kujipatia isivyo halali dola milioni 6 za Marekani, sawa na Sh bilioni 12.

Awali, upande wa mashitaka uliiambia Mahakama kuwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 Dar es Salaam, washitakiwa hao walipanga kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.

Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 kwenye makao makuu ya benki ya Stanbic Tanzania Limited, Kinondoni, Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya benki ya Standard Agosti 2, 2012. Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walipandishwa kizimbani Aprili mosi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo