Polisi wawapiga ‘stop’ mgambo Dar


Salha Mohamed

Lucas Mkondya
MKUU wa Operesheni wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, amepiga marufuku askari wa mgambo kufanya kazi kwenye vituo vya Polisi, badala yake wafanye kazi zao ngazi ya serikali za mitaa na kata.

Pia ametoa onyo kwa baadhi ya mgambo wasio waaminifu na kwenda kinyume cha sheria na utaratibu, kwa kunyanyasa wananchi kwa kuwaomba rushwa na kuvitumia vituo hivyo kwa nia ovu.

Mkondya alisema hayo wakati wananchi wa kata ya Yombo, mtaa wa Machimbo, Temeke, kutoa changamoto ikiwamo ya kunyanyaswa na askari Polisi.

Wananchi hao, walilalamikia kukithiri vitendo vya uhalifu, kiasi cha kuishi kwa hofu, ikiwa ni pamoja na kufunga biashara zao saa 12 jioni.

Walisema eneo hilo kumekuwa kukisikika milio ya bunduki na kuwa kitu cha kawaida huku ujambazi, uvamizi wa vikundi vinavyojiita Panya road na Mbwamwitu vikiwakosesha usingizi.

Walisema wamekuwa wakikosa huduma stahiki katika kituo cha Polisi cha Sigala, eneo hilo huku wakiwatuhumu baadhi ya askari Polisi kuomba rushwa.

“Tunanyanyasika na watu wasio na silaha kwa nini? Mbona tunanyanyasika hivi?” Alihoji Josephat Charles mkazi wa eneo hilo huku akilalamikia kamatakamata ya Polisi katika eneo la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akijibu changamoto hizo, Kamanda Mkondya aliwataka wananchi kuwataja bila woga polisi wanaojihusisha na vitendo viovu.

Hata hivyo, Mkondya alisema hali hiyo pia inachangiwa na mwingiliano wa mgambo na askari jamii ambao hutumia vituo vya Polisi.

Alisema baadhi ya mgambo na askari jamii hao si waaminifu na hujifanya polisi kwa kuwa hutumia vituo vya Polisi kufanya shughuli zao.

“Ndiyo maana raia wakifika katika vituo vyetu vya Polisi na kuhudumiwa na mgambo au askari jamii huombwa rushwa au kunyanyaswa na shutuma zote kwenda Jeshi la Polisi.

 “Ni marufuku kwa mgambo wala ulinzi shirikishi kufanya kazi zao kwenye vituo vya Polisi. Wafanye kazi zao katika ofisi zao za serikali za mitaa au kata,” alisema.

Alisema mgambo wanatakiwa kukamata watuhumiwa na kuwafikisha na kuwakabidhi katika vituo vya Polisi wao kurejea ofisi za serikali za mitaa au kata.

Aidha, Mkondya alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto kuendesha gwaride kwa askari wa kituo cha Polisi cha Sigala kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh 50,000 kwa mkazi wa eneo hilo, Yusta Makini ambaye alidaiwa mtoto wake kukamatwa eneo la Tanesco akienda dukani kununua vocha na kutakiwa kutoa kiasi hicho ili aweze kuachwa huru.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Simon Ngonyani juzi aliingia kwenye mkono wa sheria baada ya Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kumkabidhi kwa Kamanda Muroto ili aeleze kwa kina sababu za kifo cha mwananchi livyeuawa katika eneo lake.

Hatua hiyo ya Mwenyekiti huyo wa mtaa ilisababisha kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha mbele ya Makonda: 

"Mkuu wa Mkoa wakati napigiwa simu kujulishwa hiyo taarifa simu yangu ilikuwa imezima na ipo kwenye chaji," alisema na kabla ya kuendelea Makonda alimkatiza:

"Hatutaki kusikia hadithi za simu tunataka utueleze unafahamu nini kuhusu kuuawa kwa mwananchi huyo katika eneo lako au hufahamu?

"Sijaridhika na maelezo ya huyu mtu, Kamanda mchukue ukamhoji ili ifahamike undani wa kifo cha mwanachi, hatutaki watumishi wasio na ushirikiano.” 



Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo