Mameya, wenyeviti wa halmashauri wabanwa


Moses Ng’wat, Mbeya

Simbachawene
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza kuwachukulia hatua kali mameya wa majiji, wenyeviti wa halmashauri za miji na wilaya, madiwani na watendaji wa halmashauri nchini, watakaobainika kutumia magari ya halmashauri kwa shughuli zao binafsi.

Pia, imewaonya viongozi hao kuacha mara moja tabia iliyoibuka ya kuchagua ama kupendekeza kuendeshwa na baadhi ya madereva wanaoweza kutekeleza matakwa yao na kuwakataa madereva wanaosimamia taaluma zao na utumishi wa umma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, Ameichiory Biyengo alibainisha hayo juzi alipokuwa akisoma waraka mahususi kutoka Tamisemi kuhusu matumizi ya magari ya halmashauri wakati wa kikao cha baraza la madiwani.

“Maelekezo ya barua hii yasomwe  kwenye mabaraza ya madiwani kwa kuwa waheshimiwa madiwani ndio wasimamizi wakuu wa mali za halmashauri ili wao wenyewe waongoze katika utunzaji wa mali hizo na waweze kusimamia ipasavyo utekelezaji wa maelekezo haya,” Biyengo alinukuu sehemu ya waraka huo.

Kwa mujibu wa waraka huo, Tamisemi imechukua hatua hiyo baada ya kupokea maombi mbalimbali ya magari kutoka kwa wakurugenzi wa halmashauri kufuatia kukabiliwa na upungufu wa vitendea kazi kulikosababishwa na uchakavu wa magari na sababu nyingine.

“Pamoja na maombi hayo, uchunguzi uliofanywa na ofisi hii, umebaini kuwa uchakavu wa magari ya halmashauri unatokana na matumizi mabaya ya magari kwa viongozi wa siasa na maofisa waliopewa dhamana ya kuyatumia magari hayo vibaya kwa shughuli binafsi, ” ilinukuu sehemu ya waraka huo.

Katika waraka huo wa Oktoba 12 mwaka huu na kusainiwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Mussa Iyombe umewataka wakurugenzi wote wa halmashauri za majiji, miji na wilaya kuusoma waraka huo kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani  kwa kuwa wao ndio wenye dhamana ya kusimamia mali za halmashauri.

“Ipo tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa na watumishi wa Halmashauri kutumia magari ya halmashauri kwa shughuli zao binafsi, hali hii inasababisha viongozi hao kuchagua ama kupendekeza kuendeshwa na baadhi ya madereva ambao wanaweza kutekeleza matakwa yao na kuwakataa madereva wanaosimamia taaluma zao na za utumishi wa umma.”

Waraka huo pia unaagiza shughuli zote za upangaji wa magari kwa madereva katika halmashauri nchini ufanyike kwa kuzingatia weledi wa taaluma na si upendeleo  au maslahi binafsi ya kiongozi husika .

Kutokana na hali hiyo Tamisemi imesema haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu na kisheria kiongozi au mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 na Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo