Sitta aliyemgomea Mwalimu Nyerere na kuja kuwa Spika


Mwandishi Wetu

Marehemu Samuel Sitta
ILIKUWA Desemba 18 mwaka 1942 wilayani Urambo mkoani Tabora, ndipo alizaliwa Hayati Samuel John Sitta, Spika wa Bunge la Tisa.

Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”.

Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora (Tabora Boys), kidato cha kwanza hadi cha sita.

Baada ya kuhitimu sekondari, Sitta alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kusomea Shahada ya Sheria (LLB) mwaka 1964.

Sitta alisoma shahada hiyo kwa miaka saba kati ya mwaka 1964 na 1971, baada ya kufukuzwa chuoni hapo mwaka 1966 alipokuwa mwaka wa pili; akiwa kiongozi wa wanafunzi chuoni hapo, wakati wanafunzi walipogoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya mafunzo ya JKT.

Samuel Sitta, Wilfred Mwabulambo na wengine kadhaa waliokuwa mstari wa mbele kutetea walichokiita haki zao, waliishutumu Serikali ya wakati huo wakisema; “…ni heri wakati wa Ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu Nyerere.”

Kutokana na kauli hiyo, Rais wa Tanzania wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alikasirishwa na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao.”

Hata hivyo, baada ya mgomo na shinikizo hilo la wanafunzi, Mwalimu Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh. 4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili.

Miezi miwili baadaye, akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao waliopinga kukatwa mishahara yao wakati mawaziri wakiwa na mishahara mikubwa.

Miezi kumi baadaye, baada ya Mwalimu Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia aliamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392, lakini Sitta na wenzake saba hawakurejeshwa chuoni.

Hata hivyo, viongozi wa chuo hicho walitumia busara kuandikiwa barua mbili maalumu mwaka 1967 kwa Mwalimu Nyerere, kumuomba awarejeshe chuoni wanafunzi hao.

Kuchapwa viboko na Nyerere

Baada ya barua hizo, hatimaye, Mwalimu Nyerere aliwarejesha chuoni Sitta na  wenzake saba kwa sharti, yeye mwenyewe awatandike viboko  Sitta na Mwabulambo, ambapo walitii adhabu hiyo na kurejea chuoni  kuendelea na masomo hadi walipohitimu mwaka 1971.

Hata hivyo, Sitta alirejea chuoni akiwa tayari mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “Caltex” akiwa Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975, aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kuwa Katibu na Mkurugenzi wa Utawala.

Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE, ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huo huo 1976.

Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta amekuwa kiongozi wa juu wa CCM na Serikali akiwa Mbunge, Mkuu wa Mkoa na Waziri kwa nyakati tofauti; nafasi alizoshika hata baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kuanzia mwaka 1975 - 1995 enzi za mfumo wa chama kimoja, Sitta alikuwa Mbunge wa Urambo (kabla jimbo hilo halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alikuwa Waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.

Kuangushwa jimboni

Mwaka 1995, Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR-Mageuzi.

Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.

Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 ambapo kwenye Uchaguzi Mkuu aliwashinda wapinzani wake wakuu; Lumatiliza Lubungila wa NCCR-Mageuzi na Wilson Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660 (asilimia 72.3) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki.

Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio.

Kurejesha heshima

Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 sawa na asilimia 70.47.

Sitta alipoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.

Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010, alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kuwa Waziri, wadhifa aliodumu nao hadi mwaka jana mwanzoni alipobadilishwa na kupelekwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.

Mbio za urais

Sitta alianza mbio za urais ‘kimyakimya’ tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010) maana kuna nyakati alikuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti, huku akionesha kuwa viongozi thabiti waliopo hawajapewa uongozi, akiwemo yeye.

Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa mara kwa mara, juu ya urais alionesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa, alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.

Sitta aliingia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu ambapo jina lake halikufika kwenye Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), hiyo ikawa ndio mwisho wake kisiasa kwani hajawahi kuonekana katika harakati hizo tangu kipindi hicho.

Changamoto za afya

Baada ya kimya kirefu, taarifa zilianza kusambaa kuwa afya yake si nzuri na baadae akasafirishwa kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu ambapo usiku wa kuamkia jana alifariki.

Kwa mujibu wa mwanae ambaye ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta, baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.

Alisema Marehemu Sitta aligundua ugonjwa huo ukiwa umeathiri sehemu kubwa ya mwili hivyo ikashindikana kutibika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo