Kesi ya rushwa ya vigogo bandarini yapigwa kalenda


Grace Gurisha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi ya kuomba rushwa inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na wenzake haujakamilika.

Katika kesi hiyo, Mgawe na wenzake wanadaiwa kuomba rushwa ya ya dola za Marekani milioni nne sawa na zaidi ya Sh bilioni nane kupitia   wakala wa Kampuni ya DB Shapriya, ili kuiwezesha kampuni hiyo  kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji Mwemaya, Kigamboni Dar es Salaam.

Kutokana na kutokamilika kwa ushahidi huo, Wakili wa Takukuru, Emmanuel Jacob jana aliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Baada ya Jacob kudai kuwa upelelezi haujakamilika, hakimu alikubaliana na ombi lao na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30 kwa kutajwa. 

Mbali na Mgawe, vigogo wengine wanashitakiwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa zamani wa Uhandisi wa TPA, Bakari Kilo (59), aliyekuwa Meneja wa Mazingira wa TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).

Jacob alidai kuwa kosa la kuomba rushwa linamkabili Mgawe, Kilo na Kimaro; ambao kwa pamoja wanashitakiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti na maeneo tofauti ambayo hayafahamiki kati ya mwaka 2009 na 2012.

Ilidaiwa kuwa kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ili Shapriya ashinde zabuni iliyokuwa ikishindaniwa yenye namba AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo katika rasi ya Mjimwema, ambapo likijengwa meli zinaweza kupita juu ya pomba hilo.

Katika kosa la pili, linalomkabili Shapriya peke, mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009; akiwa   Mkurugenzi wa DB, alitoa rushwa ya dola za Marekani milioni nne kwa vigogo hao.

Inadaiwa kuwa rushwa hiyo ilitolewa ili kushawishi kuiwezesha kampuni ya Leighton Offoshore Pte, kupata zabuni ya ujenzi wa Bomba la Kupakulia Mafuta kwenye  rasi  ya Mji Mwema ya TPA.

Shapriya anadaiwa alitoa kiasi hicho kwa Mgawe, Kilo na Kimaro kwa ajili ya kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni namba AE/0116/2008-2009/10/59 ya ujenzi huo wa bomba hilo la TPA katika rasi ya Mjimwema Kigamboni.

Vigogo hao walinusurika kwenda rumande baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu waliosaini bondi ya Sh milioni 500 kwa kila mmoja.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo