Kafulila amkimbia Danda uchaguzi NCCR


Fidelis Butahe

WAJUMBE 47 kati ya 71  wa mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi juzi usiku walimchagua Danda Juju kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho.

Danda ambaye kwa takribani miaka mitano alikuwa msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia, aliibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika kuziba nafasi tatu zilizokuwa wazi, ikiwemo ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe aliyejiuzulu hivi karibuni.

Uchaguzi huo uliojaa kila aina ya mvutano na maneno ya hapa na pale, ulimalizika saa 4:10 usiku, huku aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliyejitosa kuwania ukatibu mkuu, akijitoa dakika za mwisho na kuzua minong’ono miongoni mwa wajumbe.

Kafulila ambaye ameanguka katika kesi ya kupinga ushindi wa mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima, alikuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi ya chama hicho.

Kwa ushindi huo, Danda anakuwa Katibu Mkuu wa saba wa chama hicho tangu kilipoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 90.

Mbali na Danda, chama hicho pia kilichagua Naibu Katibu Mkuu Bara na Mweka Hazina.

Akizungumza na JAMBO LEO, Mkuu wa Idara ya Organaizesheni na Utawala wa chama hicho, Florian Rutayuga alisema: “Wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu wapo 84, lakini waliopiga kura walikuwa 71. Kafulila alijitoa dakika za mwisho, baada ya kuitwa kuhojiwa kama walivyofanya wenzake. Baada ya kujitoa Danda alipambana na Faustine Sungura ambaye alipata kura 24.”

Alisema kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Bara, Elizabeth Mhagama aliibuka mshindi, baada ya kupata kura 67 na kuwashinda, Hassan Mlage (4) na Hassan Luanya ambaye hakupata kura hata moja.

“Kwa mweka hazina, Mike Kalava alishinda baada ya kupata kura 52 huku Beati Mpitabakana akipata kura 19,” alisema.

Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, Danda atalazimika kupendekeza majina ya wakuu tisa wa idara za chama hicho kwa ajili ya kupitishwa na mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa.

Waliowahi kuwa makatibu wakuu wa chama hicho ni Mabere Marando, Prince Bagenda, Dk Ringo Tenga, Mwaiseje Polisia, Samwel Ruhuza na Nyambabe.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo