JPM akata mirija 10



MWAKA MMOJA 

*Ni iliyokuwa ikitumiwa kwa ulaji, dili
*Aombwa ajielekeze Escrow, Lugumi

Fidelis Butahe

Rais John Magufuli
SIKU kama ya leo mwaka mmoja uliopita, Watanzania walikuwa wakisubiri kwa hamu matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyomweka madarakani Rais John Magufuli ambaye katika kipindi cha takribani mwaka mmoja wa uongozi wake, anatajwa kukata mirija 10 ya ulaji, JAMBO LEO linachambua.

Rais huyo wa Awamu ya Tano ambaye aliapishwa Novemba 5 mwaka jana, amekuwa akieleza mikakati yake, ikiwamo ya kubana matumizi ambayo baadhi ya wananchi wanaieleza kusababisha ‘kukausha’ fedha mifukoni na kwamba sasa hali ni ngumu zaidi.

Wakati ubanaji huo wa matumizi ukigeuka kilio kwa baadhi ya wananchi ambao Rais amekuwa akisisitiza wafanye kazi ili kuzipata kwa sababu za bure bure hazipo kwenye utawala wake, hali imekuwa tete zaidi kwa wapiga dili na waliotumia mgongo wa Serikali kujipatia fedha kinyume na taratibu.

Wachambuzi waliozungumza na JAMBO LEO mbali na kupongeza hatua zilizochukuliwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi katika kipindi chake kifupi cha utawala, wakimtaka kushughulikia vigogo ‘wapiga dili’ lakini walitaja kasoro waliyoibaini kuwa ni ya kuminya demokrasia.

Walitaja baadhi ya maeneo ambayo Dk Magufuli hajayagusa na vigogo wanatajwa kuhusika ni; mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises inayodaiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, wizi wa fedha kutoka akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) na mgawo wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, mirija iliyozibwa na Rais Magufuli tangu aingie madarakani ni; malipo ya watumishi hewa, mapato ya taasisi za udhibiti kwenda mfuko mkuu wa Serikali, kuzuia taasisi na idara za Serikali kufanya mikutano na makongamano nje ya kumbi zao, kuziba mianya ya rushwa bandarini na uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na kufuta sherehe mbalimbali za kitaifa.

Nyingine ni kiinua mgongo cha wabunge kukatwa kodi, maduka binafsi kuondolewa katika hospitali za serikali, kufuta safari za nje na kuondoa utaratibu wa kuuzia askari na wanajeshi bidhaa zisizolipiwa kodi kupitia maduka maalumu kwenye kambi za majeshi.

Maoni   

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema: “Amerejesha imani ya Serikali kwa wananchi maana awali tulikuwa tunajiuliza kuna Serikali au hakuna…, ameonesha kuwa mfumo mzuri wa uongozi kwenye taasisi hauwezi kutosha bila usimamizi na ufuatiliaji unaoeleweka.

“Hatua zake za kubana ubadhirifu bandarini na kuishukia Wizara ya Fedha na Mipango, zilikuwa na maana. Ila katika hili la kubana demokrasia watu lazima waelewe kuwa demokrasia lazima iambatane na utii na uwajibikaji.”

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha aliungana na Dk Bana, lakini akipinga kuhusu demokrasia kwa maelezo kuwa, uamuzi wa Rais kuzuia mikutano ya kisiasa ni sawa na kuzuia Watanzania kujua jinsi nchi yao inavyotafunwa.
Alisema wapinzani nao wana nafasi kubwa ya kufichua maovu na ulaji unaofanywa na wachache serikalini, na kumwomba Rais alitafakari upya katazo hilo.

“Ukitazama EPA, Escrow na hata Lugumi, ni kashfa ambazo kwa kiasi kikubwa ziliibuliwa na wapinzani na nyingine ni katika mikutano ya hadhara,” alisema.

“Rais amebana matumizi, amerejesha uwajibikaji, amepambana na watumishi hewa, ufisadi na rushwa, ingawa bado naliona tatizo katika kushughulikia vigogo waliohusika katika kashfa mbalimbali, mfano ni ile ya Escrow.”

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema utawala wake wa mwaka mmoja umeonesha mafanikio katika baadhi ya mambo, licha ya kuwa hajabana vigogo sawasawa.

“Haina maana kama anatatua changamoto ndogo anaacha mambo makubwa kama Lugumi na Escrow… tunataka ayashughulikie ili tuamini kuwa ana dhamira ya kutukomboa,” alisema.

Alisema Rais anapaswa kuongeza juhudi katika sekta za elimu na afya ambazo bado zina changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Alibainisha kuwa Rais anatakiwa kutambua kuwa mafanikio yoyote yanahitaji ushirikiano wa pande zote na si kwa mfumo wa ubaguzi ambao unasababisha malalamiko.

Mbunge Viti Maalumu CUF,  Salma Mwasa alisema jitihada za Rais tangu aingie madarakani hazijatoa mwelekeo kwa wananchi, hivyo anapaswa kujitathmini upya.
Alisema hali ya maisha ya wananchi ni ngumu isiyoendana na hatua alizochukua tangu aingie madarakani.

“Unaona jinsi Rais na wasaidizi wake wanavyotumia Jeshi la Polisi kuminya demokrasia, kimsingi uamuzi huo unapunguza uaminifu kwa wananchi licha ya kupenda matamshi kuwa anapenda Watanzania wote,” alisema Mwasa.

Watumishi hewa

Katika sherehe za Mei mosi zilizofanyika kitaifa Dodoma, Rais Magufuli alisema mpaka wakati huo watumishi hewa walikuwa  10,295 kwa mwezi wakilipwa Sh bilioni 11.63, na kutoa mfano kuwa kama fedha hizo zingetumika katika maendeleo zingejenga madaraja matatu kama la Nyerere la Kigamboni, barabara za juu saba kama zinazojengwa Dar es Salaam.

Huenda fedha hizo zilikuwa zikitafunwa na wachache kabla ya kubainika.

Sherehe

Mbali na agizo lake la kutaka viongozi wa Serikali walioalikwa kwenye kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kurejesha posho walizopewa, Novemba 8 mwaka jana, ikiwa ni siku tatu baada ya kuapishwa, Rais alitangaza kuokoa Sh milioni 225 zilizochangwa kugharimia hafla ya wabunge na kuagiza zinunulie vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Pia alifuta sherehe za Uhuru za Desemba 9 mwaka jana na kuamuru Sh bilioni 4 zilizokuwa zitumike, zipelekwe kupanua barabara ya Morocco-Mwenge.
Pia alifuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi na kuagiza fedha zilizopangwa kutumika, zikanunulie dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV).

Rais pia aliahirisha sherehe za Muungano Aprili 26 na kuokoa Sh bilioni 2 na kutaka zitumike kupanua barabara ya Ghana hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Safari

Novemba 7 mwaka jana, Rais alitangaza kufuta safari za nje ya nchi hadi uamuzi mwingine utakapotolewa. Alisema shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaowakilisha Tanzania nchi za nje na watakaosafiri ni kwa vibali maalumu.

Uamuzi huo ulionekana kuziba mianya ya baadhi ya viongozi kujipatia fedha zilizokuwa zikitengwa kwa ajili ya safari.

Mikutano  

Katika hotuba yake bungeni Novemba 20, mwaka jana Rais alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi, zikiwamo za warsha, semina, makongamano na matamasha kufanyika katika kumbi za taasisi za Serikali au wizara.

Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa ilisababisha baadhi ya hoteli kupoteza wateja wa uhakika, ambao ni taasisi za Serikali.

Bandari

Mara baada ya kuchaguliwa, Rais Magufuli mara kwa mara amekuwa akifanya ziara kwenye bandari ya Dar es Salaam, sambamba na kuwachukulia hatua watendaji waliobainika kuwa na tuhuma, zikiwamo za kutafuna mabilioni ya fedha.

Mpaka sasa takriban watumishi 50 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamefukuzwa kazi.

Usafirishaji

Mbali ya hatua alizochukulia watendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na wa viwanja vya ndege nchini kutokana na tuhuma, hivi karibuni aliagiza kufanyika uchunguzi wa gharama za upanuzi wa uwanja wa ndege wa JNIA, baada ya kubaini upanuzi wake kugharimu zaidi ya Sh bilioni 7.

Wabunge
Uamuzi wa Rais kutaka kiinua mgongo chake kukatwa kodi sambamba na kutaja mshahara wake wa Sh milioni 9.5, ulikuwa mwanzo wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutangaza mpango wa Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/17,  kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge, ambao awali walikuwa hawakatwi.

Maduka  

Mkakati wa Wizara ya Afya kukomesha wizi wa dawa unaofanywa na watumishi wasio waaminifu kwa kuandaa mkakati wa kuondoa maduka binafsi ya dawa kwenye hospitali za Serikali, lilikuwa ni pigo lingine lililobana ulaji wa baadhi ya watu na watendaji wa Serikali wasio waaminifu.

Mapato

Ulaji mwingine uliobanwa baada ya Serikali mwaka 2016/17 kuamua mapato ya taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Mafuta (Ewura), Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine za udhibiti, kupelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ambako mahitaji ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa na mapato yaliyokusanywa.

Majeshi  

Katika mwaka 2016/17 wa fedha, maduka ya kutoa huduma kwa askari yalifutiwa kodi na badala yake Serikali inajipanga kuongeza posho kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na ofisi zote za Serikali, zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni asiyetumia mashine za kukusanyia kodi (EFD).

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo