Baraza la Vyama lalia faulo ya kisiasa

Suleiman Msuya

Peter Mziray
BARAZA la Vyama vya Siasa nchini limesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Serikali vina dhamira ya kuua vyama vya siasa nchini.

Kauli hiyo ya Baraza imetolewa na Mwenyekiti wake, Peter Mziray wakati akizungumza na JAMBO LEO jana kwa njia ya simu siku chache baada ya kurejea nchini.

Mziray alisema kwa muda mrefu Baraza limekuwa likiomba vikao vya wajumbe wake ili kuzungumza na kutatua changamoto linazokabiliana nazo za kisiasa ila ofisi hiyo imeshindwa kuviwezesha.

Alisema hali ya kisiasa nchini si nzuri, hivyo wajumbe wamekuwa wakihoji sababu ya kutokutana hali ambayo inampa wakati mgumu akiwa Mwenyekiti.

“Serikali hii haitaki vyama vya siasa kabisa, kwani kila tukifanya jitihada za kutukutanisha tunakwama na ninachoona hapa kikwazo ni Mwenyekiti,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema ni jambo la kushangaza kuona Rais John Magufuli anaonekana kuchukia vyama vya siasa huku akitokana na vyama hivyo hivyo.

Mziray alisema iwapo hakutakuwa na uwezekano wa wao kukutana wataandaa mkutano hata chini ya mwembe kwani bila vyama kukukutana vinaweza kufa.

Alisema kitendo cha vyama kutofanya mikutano ni kuua vyama vikubwa kama CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, hivyo kuitaka Serikali kuachana na utaratibu huo wa kuzuia siasa.

Mziray alisema wakati ofisi hiyo ikishindwa kuwapa fedha za kuandaa vikao vya wajumbe, imetoa barua ya kutaarifu vyama vya siasa kuhusu nia yake ya kufanya ziara za kukagua vyama ngazi za wilaya.

Akizungumzia hali hiyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema malalamiko hayo hayana ukweli na kuweka bayana kuwa Baraza hilo limekuwa likikutana kupitia Kamati ya Uongozi.

“Kama sijakosea, wakati wa harakati za Umoja kwa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) Kamati ya Uongozi ilikutana, hivyo si sahihi kusema hatujafanya vikao labda aseme lingine,” alisema.

Nyahoza alisema sababu ya kutoitisha vikao vingine kwa siku za karibuni, Baraza hilo linatarajia kufikia kikomo mwezi huu hivyo watakutana kujadiliana na kufanya uchaguzi wa uongozi mpya.

Alisema ofisi yake haina nia yoyote ovu ya kuua vyama vya siasa kwa kuwa vyama hivyo vipo kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo