Wanafunzi wote kupewa mikopo kesho


Hussein Ndubikile

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema wanafunzi wote wa elimu ya juu wanaostahili mikopo watapewa ndani ya saa 72 kuanzia jana.

Pia amebainisha kuwa Serikali imeongeza kiwango cha bajeti ya mikopo kutoka Sh bilioni 340 hadi Sh bilioni 483 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu kilipoanzishwa Oktoba 25, 1961.

Alisema kuanzia juzi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini, ilianza kuwapa mikopo wanafunzi wachache huku akisisitiza kuwa kufikia kesho asilimia 90 ya wanafunzi wanaostahiki mikopo watapewa.

"Wachache sana jana (juzi) walianza kupewa mikopo, kufikia keshokutwa (kesho) Serikali itawapa mikopo asilimia 90 ya wanaotakiwa kupata," alisema.

Majaliwa alisema Serikali haitavumilia ucheleweshaji wa makusudi wa fedha utakaofanywa na Mamlaka husika, huku akieleza taasisi za elimu kufikisha taarifa sehemu husika ili kuepuka migogoro ya wanafunzi na Serikali yao.

Aliongeza kuwa hadi Oktoba 20 Serikali ilifanya uhakiki wa wafanyakazi 16,500 na baada ya mchakato huo uhakiki wa malimbikizo ya madeni ya watumishi wa chuo hicho utafanyika ili walipwe stahiki zao kwa wakati.

Alisema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wakiwamo wahadhiri waandamizi watakapohitajika na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kusaidia uendeshaji wa taasisi za umma.

Alifafanua kuwa Serikali imeshaonesha nia ya dhati ya kukabiliana na changamoto za miundombinu zinazokikabili chuo hicho, ikiwamo mahali pa kulala wanafunzi, vitendea kazi vya maabara kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni 3,840 unaoendelea.

Alipongeza mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Baraza lake la Mawaziri kwa kufanikisha kuanzishwa chuo hicho, lengo lake likiwa ni kupambana na changamoto za ujinga, maradhi na umasikini.

Pia katika maadhimisho hayo, Waziri Majaliwa alizindua kitabu cha Lumumba Street To the Hill and Beyond kinachoelezea jinsi chuo kilivyoanzishwa, maono na viongozi walioshiriki kukianzisha.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema Sh bilioni tisa zimetengwa na Wizara kushughulikia matatizo ya miundombinu ya chuo hicho na mchakato wa kuhakikisha fedha zinapatikana unaendelea.

Dk Akwilapo alisema ujenzi wa mabweni utakamilika mwishoni mwa mwaka, huku akibainisha kuwa yatapokamilika yatapunguza tatizo la malazi kwa kiasi kikubwa.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema chuo kilianza na udahili wa wanafunzi wachache ambapo   sasa kinadahaili zaidi ya wanafuzi 13,000, hivyo tangu kianzishwe kimetoa mchango mkubwa wa kuzalisha wanataaluma 90,000 walio serikalini na taasisi binafsi.

Alisema licha ya Serikali kuendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazokikabili bado kina uhaba wa rasilimaliwatu kutokana na usitishwaji wa ajira, malimbikizo ya madeni ya watumishi, vitendea kazi vya maabara na uhaba wa wahadhiri waandamizi.

Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mwanzoni wa chuo hicho, alisema wakati akiwa chuoni hapo masomo yaliyokuwa yakifundishwa yalikuwa machache na miundombinu ya majengo michache, huku akikipongeza kwa kufanya juhudi za dhati kuzalisha wasomi wanaolitumikia Taifa.

Mwanasheria na Katibu wa Chuo hicho, Profesa Palamagamba Kabudi alisema chuo kilianza na wafanyakazi sita na wanafunzi 14 wakiwamo Peter Kilabani, Gerald Kakubu, Samweli Kimwiti na Arnold Kileo huku majengo yaliyokuwa yakitumika kufundishia yakiwa ya chama cha TANU, Mtaa wa Lumumba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo