CUF yajipanga kuzuru nchi nzima


Suleiman Msuya

Maalim Seif Sharif Hamad
KAMATI Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF) imepitisha ratiba ya ziara za ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa chama kwa kanda zote itakayoongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho.

Taarifa uliyotolewa jana na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Mbarala Maharagande ilisema ziara hiyo itaanza hivi karibuni katika kanda zote saba.

Alizitaja kanda hizo kuwa ni ya Ziwa, Kati, Pwani, Nyanda za Juu Kusini, Kusini, Kaskazini na Magharibi.

Maharagande alisema Kamati kuu inawataka viongozi na wanachama kujiandaa kwa wakati.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF wajibu wa Kamati hiyo ni; “kuhakikisha chama wakati wote kinakwenda na wakati katika uhusiano, mawasiliano na utendaji wa kisayansi na uyakinifu na kinatekeleza kazi za kila siku.”  

Aidha Kamati hiyo ilipokea na kujadili hali ya kisiasa na matukio yaliyojitokeza hususan kwa madiwani wa CUF Tanga kushiriki na au kutoshiriki katika uendeshaji wa shughuli za halmashauri ya manispaa hiyo na ilichukua suala hilo kwa uzito mkubwa.

Kaimu Naibu Mkurugenzi huyo alisema Kamati kuu iliagiza suala hilo kushughulikiwa kwa uharaka kwa kuunda kamati ya kitaifa ya kulisimamia.

“Hivyo Kamati kuu inawataka wanachama wa CUF Tanga na nchini kwa ujumla, na wapenda mabadiliko kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho suala hilo linatafutiwa ufumbuzi sahihi na chama,” alisema.

Kamati pia ilitoa pongezi kwa viongozi wa chama ngazi zote, wanachama, wapenzi wa CUF na wananchi kwa ujumla ambao wameendelea kuwa madhubuti, kusimamia ajenda muhimu za chama.

Alisema wana CUF na wananchi wako pamoja na hawakubali kuyumbishwa na watu wachache wenye dhamira ovu ya kutaka kuwatoa kwenye ajenda muhimu ya kudai haki, usawa na mabadiliko ya kisiasa nchini. 

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo