Vigogo Bandari kizimbani kwa rushwa ya bil. 8/-


Grace Gurisha

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imempandisha kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na vigogo wengine watatu wa Mamlaka hiyo wakidaiwa kuomba rushwa ya dola milioni nne za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni nane.

Vigogo hao wanadaiwa kudai na kupokea rushwa hiyo ili watoe zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta.

Mbali na Mgawe, vigogo wengine ni Mkurugenzi wa zamani wa Uhandisi TPA, Bakari Kilo (59), aliyekuwa Meneja wa Mazingira TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).

Vigogo hao walipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiana na Wakili wa Takukuru, Emmanuel Jacob walidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Jacob alidai kuwa mashitaka ya kuomba rushwa yanawakabili Mgawe, Kilo na Kimaro, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti na maeneo tofauti ambayo hayafahamiki kati ya mwaka 2009 na 2012.

Ilidaiwa kuwa kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ya dola milioni nne kupitia wakala wa kampuni ya DB Shapriya ili kuiwezesha kampuni hiyo kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji Mwema ya TPA kinyume na sheria ya Takukuru.

Alidai walifanya hivyo ili Shapriya ashinde zabuni iliyokuwa ikishindaniwa namba AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo kwenye rasi ya Mjimwema.

Katika mashitaka ya pili dhidi ya Shapriya peke yake, ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009 akiwa Mkurugenzi wa DB Shapriya, alitoa rushwa ya dola milioni nne kwa vigogo hao, ikiwa ni kishawishi kuiwezesha kampuni ya Leighton Offshore Pte kupata zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji Mwema.

Inadaiwa mtuhumiwa alitoa kiasi hicho cha dola kwa Mgawe, Kilo na Kimaro ili kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni hiyo.

Baada ya kusomewa mashitaka, walikana kuhusika. Wakili Jacob alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa na pia kuwa hawana pingamizi dhidi ya dhamana.

Vigogo hao walinusurika kwenda rumande baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu waliosaini bondi ya Sh milioni 500 kila mmoja kiasi hicho hicho.

Hata hivyo, Mgawe si mara yake ya kwanza kupandishwa kizimbani katika Mahakama hiyo, kwani tayari ana kesi ya matumizi mabaya ya madaraka akishitakiwa pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Hamad Koshuma.

Ilidaiwa kuwa Desemba 5 mwaka 2011, washitakiwa wakiwa watumishi wa PTA, katika utendaji wao wa kazi kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, ikiwa kwenye hatua ya mwisho ya kutolewa hukumu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo