Milioni 800/- zakarabati miundombinu Kagera


Mwandishi Wetu, Dodoma

Mohamed Mchengerwa
SHILINGI milioni 800 ndizo zilizotumika kukarabati miundombinu katib ya Sh bilioni 5 zilziotolewa kwa ajili ya waathirika wa tetemeko mkoani Kagera, imeelezwa.

Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa (CCM) alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano kati ya Kamati hiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama uliokuwa ukipokea taarifa ya madhara ya tetemeko hilo.

Alisema Serikali inaendelea kusaidia waathirika hao na kwa sasa wanafunzi wa sekondari ya Ihungo wamehamishwa shule ya Mwani ili kuendelea na masomo.

Mchengerwa alisema taarifa ambayo Kamati hiyo ilipokea ilisema wagonjwa 440 walio hospitalini wanaendelea kupata matibabu na sita wamefariki dunia.

“Wagonjwa sita wamefariki dunia hivyo idadi ya vifo kuongezeka kutoka 17 hadi 23, wananchi wanaendelea kupata huduma ukiwamo uboreshaji wa miundombinu na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) 96 wako Kagera kulinda usalama,’’ alisema Mchengerwa.

Alisema inatakiwa miaka miwili au mitatu mkoa huo kukaa sawa kutokana na maeneo mengi kuathirika na ukarabati unafanyika taratibu.

“Kamati imeshauri Serikali isimamie afya na usalama wa wananchi waliopatwa na tetemeko, kuendelea kuratibu suala hilo kwa kushirikiana na wahisani; wataalamu wa ndani watumike kufanya utafiti katika maeneo ya bonde la ufa kabla ya maafa kutokea,’’ alisema Mchengerwa.

Pia Kamati iliiomba Serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tetemeko na kujenga nyumba imara zinazostahimili mtikisiko, kuboresha kitengo cha maafa na kuanzisha vituo vya kitaifa vyenye vifaa vya kisasa vya kukabiliana na majanga.

Kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, Kamati ilishauri kuwepo sheria maalumu kusisitiza jambo hilo na kuongeza nguvu za kusimamia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ambayo imeonekana kuwa na urasimu mkubwa katika upangaji ardhi.

“Serikali imeahidi kuhakikisha CDA haiendelezi urasimu katika upangaji na ugawaji ardhi kwa matumizi mbalimbali, kwani itaanza kutumia mfumo wa elektroniki katika ununuzi wa ardhi,‘’ alisema.

 Alisema hadi sasa wizara, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi wameshapewa maeneo kwa ajili ya kujenga ofisi na watumishi wa umma, wabunge na maofisa wengine wataanza kupewa maeneo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo