Kambi za CUF sasa ni sitaki nataka


Suleiman Msuya

SITAKI nataka. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kuhusu kinachoondelea ndani ya CUF, ambapo upande mmoja ukiweka bayana kwamba upo tayari kwa mazungumzo ya kumaliza mgogoro, huku upande mwingine ukieleza hauko tayari.

Kauli hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti jana na pande hizo katika mahojiano na JAMBO LEO, siku chache baada ya upande unaotajwa kumwunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama wengine 11 na kupinga uamuzi wa Msajili kumtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF.

Wakati upande unaomwunga mkono Lipumba ukieleza kumtambua Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho na kuwa tayari kwa mazungumzo kumaliza mgogoro ndani ya chama hicho, upande wa Maalim Seif umeeleza haupo tayari kwa hilo.

Mwenyekiti wa Muda wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alisema kwa upande wao ni vigumu kufanya mazungumzo na Lipumba na kundi lake, kwa alichodai si watu wema ndani ya chama hicho.

Mtatiro alisema kwa sasa wanasubiri taratibu za Mahakama ili kuhakikisha haki inapatikana na kuwa kuzungumza na Lipumba ni aibu kwa chama na Watanzania ambao wamepoteza imani naye.

Alisema vitendo ambavyo Lipumba na kundi lake wamefanya vimesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 600 hivyo unahitajika ujasiri wa hali ya juu kuzungumza mbele ya wana CUF kuwa unahitaji kukutana nao.

“Mazungumzo na Lipumba ni jambo ambalo haliwezekani, kwanza tambua kuwa kwa sasa si mwanachama, wala kiongozi kwani alishafukuzwa na vikao halali, hivyo ili kuzungumza lazima kurejesha hoja yake kuanzia Kamati ya Utendaji Taifa, Baraza Kuu la Uongozi na Mkutano Mkuu Taifa,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uongozi alisema kwa tathmini waliyoifanya, Lipumba haungwi mkono na wanachama wengi, hivyo hana madhara yoyote anayoweza kusababisha ndani ya chama.

Aidha, alisema jambo la kufurahisha ni kuwa hadi sasa vyombo vya uamuzi ndani ya chama hicho viko upande wa chama tofauti na ilivyo kwa Lipumba ambaye anaungwa mkono na wachache wasio na uwezo wa kufanya uamuzi.

Alisema Lipumba anapata huduma kutoka Serikalini, hivyo ni vigumu kuamini kuwa watakuwa wanafanya mazungumzo na mwenzao au msaliti.

“Makao makuu ya chama yako salama na kazi zinaendelea hivyo tunachokifanya sasa ni kuandaa mikakati ya kufanya kazi katika mikoa ambako mimi nitaongoza operesheni hizo nikiwa na Katibu Mkuu Maalim Seif na viongozi wengine wacha wao wabaki na ofisi ndogo Buguruni,” alisema

Mtatiro alisisitiza kuwa katika kuonesha kuwa Lipumba hana nguvu ni kwenye mchakato wa kufungua akaunti uliokwama hivyo wanaamini kuwa mwisho wake unafika.

Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya ambaye yuko kwa Lipumba, alisema wao wako tayari kuzungumza iwapo nafasi hiyo itapatikana kwani wanachopigania ni CUF na si mtu.

Kambaya alisema katika kuthibitisha hilo, wamekuwa wakibainisha siku zote kuwa wanamtambua Katibu Mkuu Maalim Seif na kumtaka arejee ofisi za Buguruni ili wafanye kazi.

“Watu wenye busara ni lazima wasimamie misingi ya mazungumzo katika kutatua changamoto na migogoro ambayo inawakabili hivyo wenzetu wakihitaji kufanya hivyo tuko tayari,” alisema.

Mgogoro wa CUF na Lipumba ulianza Agosti miezi takribani 10 baada ya Lipumba kutangaza kujiuzulu lakini baadaye akaandika barua ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo