Viongozi vijana walivyomwangusha Rais Magufuli


Fidelis Butahe

WAKATI Rais John Magufuli akisuka serikali yake kwa kuwatumia zaidi vijana, JAMBO LEO limebaini kuwa kundi hilo limemwangusha, baada ya kulazimika kutengua uteuzi wa wateule 16 katika kipindi cha miezi minne tu tangu waanze kazi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wamesema Rais huyo wa Awamu ya Tano anafanya kazi nzuri, lakini alipaswa kuwa makini katika uteuzi wake ili kupata wasaidizi wataokwenda na kasi yake.

Julai  7 mwaka huu Rais alifanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji matano, Manispaa 21, Miji 22 na Wilaya 127 za Tanzania Bara. Kati ya wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 waliteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya.

Kati yao, wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya 11, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji mmoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa moja walikacha uteuzi huo na hivyo, kumlazimu Rais kuteua wengine 13 kujaza nafasi hizo, mwezi Septemba.

Pia, Septemba 27 mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda baada ya kubaini kuwa wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo “Kamati Maafa Kagera” kwa lengo la kujipatia fedha.

Oktoba 18, Rais pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Emmanuel Mkumbo huku Ikulu ikieleza kuwa atakayeziba nafasi hiyo atatangazwa baadaye.

Uteuzi huo ulitenguliwa ikiwa imepita siku moja tangu Mkumbo alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kwa tuhuma za kutishia kumuua askari wa usalama barabarani mkoani humo, Koplo Tuti Ndaga.

Tukio hilo lilitokea takribani wiki moja iliyopita eneo la Mkambarani baada ya mkurugenzi huyo kutakiwa  kusimama, baadaye kudai anatumia gari la Serikali licha ya kubainika kuwa na kasoro kadhaa.

Maoni ya wachambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema: “Nadhani ni kwa sababu rais ameleta watendaji wapya wengi kuziba nafasi za wazoefu…, siamini kama wakurugenzi wa zamani hawakuwa na sifa nzuri za uchapaji kazi. Siamini kama rais alikuwa na taarifa zao sahihi.”

“Miongoni mwa watendaji wa zamani, wapo ambao walipaswa kuachwa huku akiponda uteuzi wa wakurugenzi hao kufanyika kisiasa, inakuwaje watumishi wa Serikali wanakuwa makada wa chama? Hili hupunguza uwajibikaji kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema: “Kuna sababu mbili, kwanza ni rais mwenyewe na pili ni watendaji anaowateua.”

Aliongeza: “Katika jambo la kwanza naona tatizo katika kuchagua majina ya watu ambao rais anapaswa kuwateua. Ukitizama utaona sura nyingi mpya tofauti na marais waliopita ambao walikuwa na utaratibu wa kuteua wapya wachache na kuendelea na wale waliowakuta kwa ajili ya kuendeleza uzoefu.”

Alisema kinachotokea sasa ni ishara kuwa Rais Magufuli hawaamini watendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne na kutokuwa na umakini katika kuwachagua wengine kutokana na wengi kuvurunda, kufanya mambo kinyume na matakwa ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Alibainisha kuwa baadhi ya watendaji nao wana matatizo kutokana na kushindwa kuenda na kasi ya Rais aliyedai kuwa anapenda kuona wateule wake watekeleza kile anachokiamini.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alipingana na wenzake na kubainisha kuwa ni jambo jema kwa rais kuwatumbua watendaji wazembe na wanaokiuka utaratibu wa kazi aliouweka.

“Mwalimu Nyerere (Julius) aliwahi kusema zamani watendaji walikuwa hawachukuliwi hatua kwa sababu ya uchache wao. Kwa sasa wapo wengi, hivyo mmoja akiharibu ni vyema akaondolewa na kuwekwa mwingine,” alisema.

“Rais amekuwa akisisitiza kubana matumizi na kupambana na rushwa hivyo lazima awe na watendaji wanaokwenda na kasi ya kupambana na mambo hayo. Ndio maana alimwondoa Kitwanga (Charles-aliyekuwa Waziri wa Mmabo ya Ndani), kwa ulevi.”
Ends
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo