Kamati Kuu CUF yapitisha ratiba



Suleiman Msuya

KAMATI Kuu ya Utendaji Taifa Chama cha Wananchi (CUF) imepitisha ratiba ya ziara za ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa chama kwa kanda zote itakayoongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho.

Taarifa uliyotolewa na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CUF, Mbaraka Maharagande ilisema ziara hiyo itaanza hivi karibuni kwa kuzifikia kanda zote nchini ikiwemo Kanda ya ziwa, Kati, Pwani, Nyanda za Juu Kusini, Kusini, Kaskazini na Magharibi.

Maharagande alisema kamati kuu inawataka viongozi na wanachama kujiandaa na ziara hizo na kuhakikisha maandalizi yote ya msingi yanakamilika kwa wakati.

“Kamati kuu imepitisha ratiba ya ziara za ukaguzi, ujenzi na uimarishaji wa chama kwa kanda zote kwani hilo ni moja ya lengo la chama cha siasa,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF Ibara 85(1) na (3) ni wajibu wa kamati ya utendaji Taifa; “kuhakikisha kuwa Chama wakati wote kinakwenda na wakati katika mahusiano, mawasiliano na utendaji wa shughuli za Chama kisayansi na uyakinifu” na “kinatekeleza kazi za kila siku za chama ngazi ya Taifa” aliongeza.

Aidha kamati hiyo imepokea na kujadili hali ya kisiasa na matukio yaliyojitokeza kuhusiana na madiwani wa CUF katika jiji la Tanga kushiriki na au kutoshiriki katika uendeshaji wa shughuli za halmashauri ya manispaa hiyo na kwamba imelichukua suala hilo kwa uzito mkubwa.

Kaimu Naibu Mkurugenzi huyo alisema kamati kuu imeagiza suala hilo kushughulikiwa kwa uharaka kwa kuunda kamati ya kitaifa ya kulisimamia suala hilo.

“Hivyo kamati kuu inawataka wanachama wa CUF Tanga na nchini kwa ujumla, na wapenda mabadiliko kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho suala hilo linatafutiwa ufumbuzi sahihi na chama,” alisema.

Kwa upande mwingine kamati hiyo imetoa pongezi kwa viongozi wa chama kwa ngazi zote, wanachama, wapenzi wa CUF na wananchi wote kwa ujumla ambao wameendelea kuwa madhubuti, imara zaidi kusimamia ajenda muhimu za chama hicho.

Alisema hadi sasa wana CUF na wananchi wapo pamoja na hawakubali kuyumbishwa na watu wachache wenye dhamira ovu ya kutaka kuwatoa katika ajenda muhimu ya kudai haki, usawa na mabadiliko ya kisiasa nchini.

Maharagandec alisema kamati kuu imesisitiza kuwa CUF ipo imara na itaendea kuweka mipango madhubuti ya kujiimarisha ndani ya chama na kujenga ushirikiano makini na vyama rafiki katika UKAWA.

Aidha alisema kamati kuu inazipongeza taasisi za Kimataifa ambazo mara zote zimekuwa na msaada mkubwa kuwezesha ufanikishaji wa programu mbalimbali za chama ikiwemo utoaji mafunzo kwa viongozi na wanachama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo