TEMESA yaja na teknolojia ya kubaini vipuri bandia vya magari


Mwandishi Wetu, Iringa

WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umeanzisha programu ya kubaini vipuri bandia vya magari kwa ajili ya kuboresha huduma za matengenezo ya magari na mashine mbalimbali.

Hayo yalielezwa na mtendaji mkuu wa wakala huo, Dk. Mussa Mgwatu alipotembelea karakana ya TEMESA ya mkoani Iringa na kujionea jinsi karakana hiyo inavyotumia mfumo huo mpya kubaini vipuri bandia.

Dk. Mgwatu alisema kuwa mfumo huu umekuja wakati sahihi kwani kwa sasa kumekuwa na uingizwaji wa vipuri bandia vya magari ambavyo vimesababisha hasara kwa wamiliki wa vifaa vinavyotumia vipuri kutoka nje ya Tanzania.

“Ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, inabidi tuwe na mfumo ambao utatusaidia kutambua vipuri bandia, kwani vinakwamisha sana utendaji kazi wetu” alisema Dk Mgwatu.

Mgwatu ameziagiza karakana zote za TEMESA nchini kuanza kutumia programu ya kompyuta katika kuagizia vipuri toka kwa wazabuni ili kuondokana na lawama zinaotokea wakati wa kutengeneza na kukarabati magari ya Serikali na mitambo mbalimbali.

Soko la vipuri vya magari, kama yalivyo masoko ya vifaa vingine, limeingiliwa kwa kasi na uwepo wa vipuri bandia (Non genuine parts) katika kukabiliana na tatizo hili TEMESA imeamua kuanzisha mfumo wa kubaini vipuri bandia.

Akieleza jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Meneja wa TEMESA mkoa wa Iringa, Mhandisi Ian Makule alisema kuwa kwa kuingiza taarifa za namba ya gari husika kwenye programu ya kompyuta, unaweza kubaini kama kipuri kinachokusudiwa ni halisi kabla ya kukiagiza.

Mhandisi Makule aliongeza kuwa kama namba na jina la kipuri zitakuwa sahihi kwenye kasha lake lakini kipuri chenyewe sio halisi, kitaweza kutambuliwa kwa kutumia programu ya ‘barcode scanner’.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo