Upelelezi kesi ya akina Kitilya waendelea



Grace Gurisha

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya Uhujumu Uchumi,umeieleza Mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amewaeleza kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), bado inaendelea kumchunguza aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake.

Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,Cyprian Mkeha, baada ya Wakili wa washtakiwa hao Alex Mgongolwa kulalamika kuchelewa kukamilika kwa upelelezi.

"Upelelezi haujakamilika, lakini DPP ametuambia Takukuru wanaendelea kuwachunguza washtakiwa, kwa hiyo upelelezi ukikamilika watasema,"alidai Kishenyi

Akiwasilisha malalamiko hayo, Mgongolwa alidai kuwa ni miezi sita sasa wateja wake wapo gerezani bila kujua hatua yoyote ya upelelezi ulipofikia.

"Upande wa Jamhuri unaiingiza Mahakama gizani, kwa sababu kila kesi inapokuja wanadai upelelezi bado ukizingatia ni miezi sita sasa mara kwa mara wanaambiwa wanaendelea kufanya upelelezi.

"Kama walijisalimisha wenyewe na wakashtakiwa bila mabishano yoyote, kwa nini waseme upelelezi bado, kwa hiyo tunaomba watuambia wamefikia wapi, kwa sababu washtakiwa wanateseka gerezani,"alidai Mgongolwa

Hakimu alisema shauri hilo limebadilishiwa hakimu mwingine, ambapo hivi sasa litakuwa kwake, kwa hiyo wahakikishe upelelezi unakamilika ndani ya wakati ili kesi iendelee na hatua nyingine. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka huu.

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni aliyekuwa miss Tanzania wa mwaka 1996,Shose Sinare na aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo Arumeru Mashariki Sioi Solomon ambaye pia ni mkwe wa zamani wa Waziri Mkuu,Edward Lowassa wote ni wafanyakazi wa benki ya Standard.

Mashtaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali dola za Marekani milioni 6, sawa na sh bilioni 12.

Awali, upande wa mashtaka uliieleza mahakama katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 Dar es Salaam, washtakiwa hao watatu walipanga kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.

Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo Kinondoni mshtakiwa, Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ya Agosti 2, 2012. Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walipandishwa kizimbani Aprili Mosi mwaka huu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo