Ujenzi wa viwanda vidogo muafaka wa tatizo la ajira


Celina Mathew

SERIKALI imewataka watanzania wanaomiliki viwanda vidogo, vyakati na vikubwa kushiriki maonesho ya viwanda vya Tanzania yanayotarajiwa kuanza Desemba 7 hadi 11 mwaka huu katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere.

Maonesho hayo yatakayoambatana na kauli mbiu isemayo ‘Tanzania sasa tunajenga viwanda’ lengo lake ni  kuwaaminisha wananchi juu ya falsafa na dhima ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, na kuhamasisha watanzania kudhubutu kujenga viwanda kwa kuwakutanisha walioanza siku nyingi na wa sasa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema lengo la maonesho hayo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ifikapo 2025,pamoja na kujenga jukwaa la wadau wa sekta ya viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo.

Alisema pia yatatoa fursa za kutoa taswira ya juhudi za ujenzi wa viwanda kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa nchini ili kutoa hamasa kwa watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini.

Aidha alisema yatawaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma nyingine zinazotumika viwandani, kutoa semina na mijadala ya kitaalam ikihusiana na maendeleo ya viwanda nchini, kutangaza fursa za masoko ya ndani na nje na kuwezesha watafiti na wabunifu kujadiliana na wenye viwanda juu ya kuboresha teknolojia za uzalishaji na Tehama.

Nyingine ni kuwezesha vijana na wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira na masomo ya masuala ya viwanda ikiwemo kuwajengea tamaa ya kuanzisha  viwanda, kutoa fursa kwa wananchi kutambua viwanda vilivyopo na zaidi kuwajengea hamasa ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda na mamlaka husika zinazotumia maonesho hayo kutangaza fursa za uwekezaji katika mikoa yote ya Tanzania ikiwemo maeneo ya kujenga viwanda.

Alisema katika maonesho hayo wamelenga  kuwakutanisha wadau wote wa viwanda ambao ni pamoja na wazalishaji wa malighafi, taasisi zinazotoa huduma kwa wenye viwanda na zinazowezesha bidhaa kutoka kiwandani mpaka mikononi mwa watumiaji.

“Kama mnavyojua mpango wa pili wa miaka mitano unatamka wazi kuwa sekta binafsi ndiyo mhimili wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo maonesho haya mhusika mkuu ni sekta binafsi na serikali sisi ni wawezeshaji,”alisema.

Aliwataka watakaoshiriki kutembelea ofisi za mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zilizopo katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Nyerere ambao waratibu wake na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara hiyo na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Viwanda (UNIDO).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo