‘Kwanini Muswada wa Habari usiende bungeni’


Enlesy Mbegalo

Theophil Makunga
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeiomba Kamati za Bunge ya Huduma za Jamii kutowasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa 2016 katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 unaotarajiwa kuanza kesho likitaja sababu tano kutaka ombi lao litekelezwe.

Aidha, TEF limeomba muswada huo uwasilishwe kwenye mkutano wa sita utakaofanyika Februari mwakani kwa maelezo kwamba linaamini wakati huo watakuwa wamepata mwafaka wa mambo mengine ya msingi yanayohitaji makubaliano baina yao.

Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa wanaomba muda zaidi ili wadau mbalimbali pamoja na wanahabari wenyewe waweze kujadiliana kwa kina, kwani kuna vifungu na vipengele vinavyopaswa kufanyiwa marekebisho.

“Kwa hatua ambayo tumefikia hivi sasa, hili halitawezekana, kwani bado hatujakamilisha mchakato wa majadiliano na utoaji wa mapendekezo katika ngazi za taasisi zetu,” alisema

Alisema Oktoba 13 mwaka huu, TEF ilipata barua kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge ikiwaalika kufika mbele ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwaajili ya kutoa maoni kwenye muswada huo.

Alisema waliitika wito huo na kufika mbele ya kamati hiyo Oktoba 19, ila kwa kushirikiana na wadau wengine, waliiomba muda wa nyongeza kwa ajili ya majadiliano zaidi.

Hata hivyo, alisema baada ya muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni Septemba 16, walijitahidi kuanza kufanya kazi mapema kadri ilivyozekanavyo.

“Ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa muda, tuliwaarifu wenzetu katika maeneo mbalimbali nchini kusoma, kuchambua na kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” alisema Makunga.

Alisema kazi ya kusoma na kuchambua muswada huo iliyowakilishwa kwa wataalamu wa sheria, imechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kutokana na kuwapo na masuala yanayohitaji mjadala mpana kabla ya kufikia hitimisho na kuyatolea maoni.

Aidha mwaliko wa kamati uliwafikia wakiwa katikati ya mchakato wa kukusanya maoni, huku timu ya wataalamu ikiendelea kufanya uchambuzi wa hoja zilizokuwa zimetolewa na wadau wakiwamo wahariri.

Pia, alisema Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ambao umebeba maslahi ya waandishi wa habari nchi nzima ulikuwa bado katika hatua ya kukusanya maoni katika ngazi ya mikoa.

“Kwa ujumla sheria inayotugwa ina mambo mengine ambayo sisi kwa mtazamo wetu hayahitaji uharaka katika kuyafanyia uamuzi, masuala haya yanahitaji mjadala mpana wa wanataaluma wenyewe na wadau wengine,”

Katibu wa TEF, Nevelle Meena alisema wamesikitishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba kusema kuwa Bunge litaendelea na mchakato huo hata kama wadau hawako tayari.

“Tunaomba ieleweke kuwa sio dhamira yetu kukwaza utunzi wa sheria na wala hatupingi kutugwa kwa sheria hii, ila tunahitaji muda kupitia muswada h uo kwa makini kuona wapi kuna tatizo gani na liboreshweje, na hii ni kwa maslahi ya taifa,” alisema

Kamati ya Bunge yakamilisha kazi ya kupitia maoni

Wakati huohuo mwandishi wetu kutoka Dodoma ameripoti kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeeleza kuwa imemaliza kazi yake ya kupitia maoni yaliyowasilishwa na wadau, taasisi na wananchi ili kuboresha muswada huo.

Mwenyekiti kamati hiyo Peter Serukamba amesema kuwa wameyapitia maoni yaliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kuna maeneo ambayo Serikali wameyapokea na kamati inaendelea kuyafanyia kazi.

“Katika miswada ambayo wananchi wameisoma na kusikilizwa sana ni Muswada huu, maana ndio Muswada pekee ambao kwa kweli umejadiliwa sana katika vyombo vya habari; kwenye magazeti, kwenye radio na Tv kupitia vipindi maalum vya kujadili Muswada huu na maoni yao mengi yameingizwa kwenye Muswada huu,” alisema Serukamba.

Aliyataja maeneo ambayo kamati yake imefanyia kazi na kuyaingiza kwenye Muswada kama maboresho kulingana na maoni yaliyowasilishwa kuwa ni pamoja na namna ya kumtambua mwandishi wa habari, namna ya kulinda haki za waandishi wa habari, kulinda haki za wenye vyombo vya habari pamoja na kumlinda mtu yeyote katika jamii.

“Mimi na wanakamati wenzangu tunajivunia kwamba tumeandika historia hii ambayo iliwashinda wengine wote tangu mwaka 1993, sisi tumeweza kuleta Sheria nzuri ambayo itasaidia waandishi wa habari, itasaidia tasnia ya habari Tanzania na tutaanza kuwajibika kama taifa na ni mwanzo mpya kwa uandishi wa habari Tanzania,” alisema Serukamba.

Serukamba amewatoa hofu wadau wa habari juu ya kuanzishwa kwa sheria hiyo kwa kuwaasa kuusoma muswada huo ambao utaifanya tasnia ya habari kuwa taaluma.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo