Mambo matano mbele ya JPM



MWAKA MMOJA IKULU:

*Ajizatiti kuyakabili licha ya ahadi zilizomtangulia
*Atoa maagizo ya ‘kutafuna mifupa’ iliyoshindikana

Fidelis Butahe na Suleiman Msuya

HATUA ya Rais John Magufuli kumteua Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), umeelezwa kwamba unaweza kuwa ishara ya kufungua ukurasa mpya wa kuanza kupambana na mambo matano makubwa ya ufisadi lakini pia yenye maslahi kwa Taifa.

Uchambuzi wa JAMBO LEO na maoni ya wachambuzi unabainisha kuwa mambo hayo matano ambayo Rais Magufuli anatajwa kuyageukia ili kuyakabili na kuyamaliza, ni pamoja na vita dhidi ya ujangili, mikataba mibovu na usiri wao, dawa za kulevya, migogoro ya ardhi na kumaliza au kuanza upya mchakato wa Katiba mpya.

Kauli ya hivi karibuni ya Rais Magufuli kumtoa hofu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akimtaka kukamata majangili bila kujali dini, kabila wala cheo cha mtu ni ishara ya kufungua ukurasa huo wa mapambano ambayo wachambuzi wanasema yanaweza kufanikiwa.

Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais Magufuli amefanya mambo mbalimbali, ikiwamo kuvunja bodi za taasisi na mashirika ya Serikali, kuwahamisha kazi na kutengua uteuzi wa vigogo mbalimbali, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, jambo ambalo linahusishwa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa awali dhidi ya ujangili nchini.


Wadau
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Mabuba Kisena alisema ni mapema kutafsiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kushughulikia maeneo hayo na kwamba anaamini sasa anatengeneza mfumo wa uwajibikaji.

Kisena alisema changamoto ambazo zimekuwa zikilikumba Taifa katika ujangili, dawa za kulevya na mikataba, asilimia kubwa zinatokana na mfumo uliokuwapo kuruhusu mazingira ya rushwa.

”Mimi naamini akifanikiwa kunyoosha kwenye uwajibikaji wa watumishi kuanzia ngazi ya chini hadi juu, hayo yote ambayo yanaonekana kutoguswa yataguswa na matokeo chanya yataonekana,” alisema

Mhadhiri Paul Mtasigazya wa chuo hicho pia, alisema hatima ya yote yanayolalamikiwa ni Katiba mpya na ukweli kwamba Rais Magufuli amefanikiwa kufanya mambo yanayotia moyo.

“Naamini kuwa Katiba inaweza kujibu maswali yote ambayo yapo kwa sasa kwani kuwepo kwa siasa, biashara na mgongano wa kimaslahi ni mambo ambayo yatajibiwa na Katiba mpya,” alisema.

Mtasigazya alisema katika kipindi hiki ambacho bado Katiba haijapatikana, ni jukumu la Rais kufanya kazi kama timu, kwani kinyume cha hapo hawezi kufikia mwafaka wa anachokitaka.

Alisema bado kuna changamoto ya watumishi wa umma kumwelewa, hivyo wanapaswa kupewa mafunzo ili kuendana na kasi yake.

Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Zenda alisema masuala ya dawa za kulevya na ujangili ni mtandao mkubwa unaohitaji mipango iliyokamilika kuidhibiti.

Alisema pia mikataba ya nchi inapaswa kuchunguzwa kwa umakini kwani kinyume na hivyo, Serikali inaweza kuingia kwenye hasara kubwa.

“Nadhani unaona katika viwanja vya ndege na mipaka hali ilikuwa mbaya ila baada ya kuweka mashine hali imeanza kurekebika, hivyo Rais anapambana kisayansi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Zanzibar, Mussa Kombo Mussa alisema hatima ya yote yanayolalamikiwa muarobaini wake ni Katiba Iliyopendekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.

Alisema Katiba hiyo iliweza kuanisha kila kitu hivyo itamrahisishia Rais kufanikisha malengo yake kirahisi bila kutumia nguvu.

Ujangili

Rais alimtoa hofu Jenerali Milanzi baada ya kutembelea ghala la Wizara hiyo na kujionea vifaa vilivyokamatwa, yakiwamo meno ya tembo 50.

Kitendo cha Jenerali huyo kuulizwa na Rais kama ana hofu yoyote na kujibu kuwa chini ya ‘sapoti’ yake hana hofu yoyote ni ishara kuwa Dk Magufuli amejitosa kupambana na mtandao huo.

Lakini uteuzi wa Jenerali Waitara ndio unaonesha dhahiri jinsi alivyodhamiria kupambana na vigogo wa ujangili ambao wametamba kwa muda mrefu licha ya juhudi kadhaa zilizofanyika.

Februari 14 mwaka jana, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC alisema Serikali imebaini mtandao wa ujangili unaojumuisha watu 40, akiwamo tajiri maarufu mkoani Arusha, lakini haukuwekwa wazi kipindi hicho.


Mihadarati
Mtandao mwingine ambao umekuwa mgumu kufichuliwa ni wa dawa za kulevya, licha ya viongozi kueleza mara kadhaa kuwa wanawafahamu wahusika.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa njia ya kupitisha au kituo cha dawa za kulevya aina ya heroin, cocain, mandrax na morphine na mara kadhaa mizigo imekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kiwango kikubwa kukamatwa nje ya nchi baada ya kupita kwenye uwanja huo.

Licha ya watu wa kada mbalimbali kutaka Serikali kufichua mtandao huo unaodaiwa kuhusisha hata vigogo serikalini, wafanyabiashara wakubwa na vigogo wa Polisi, lakini mpaka sasa wanaokamatwa ni wanaobeba na si wenye mitandao.

Katiba Mpya
Kitendawili kingine kinachosubiri kuteguliwa na Rais Magufuli ni Katiba Mpya. Rais tayari ameshatamka wazi kuwa mchakato huo utaendelea pale ulipoishia.

Mapendekezo yaliyotolewa hivi karibuni na wadau, ni mchakato huo kuanzia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba huku wakipinga Katiba Inayopendekezwa kwa maelezo kuwa iliacha maoni ya msingi ya wananchi.

Ili mchakato wa kupata Katiba Mpya uweze kuendelea, Serikali italazimika kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, ili kuibadili iendane na wakati wa sasa kwa ajili ya kuendelea na mchakato huo ulioishia katika upigaji kura ya maoni.

Migogoro ya Ardhi

Migogoro ya ardhi nchini imekuwa chanzo cha mapigano baina ya wakulima na wafugaji na kupoteza uhai wa watu na mifugo, migogoro ya wananchi na wawekezaji na uvamizi wa maeneo yasiyoruhusiwa kwa ujenzi, yanaonekana kutopatiwa ufumbuzi.

Mara kadhaa imeelezwa matatizo hayo yanatokana na ardhi kutopimwa na kugawanywa vizuri, lakini bado hayajatatuliwa.

Maeneo yaliyokithiri kwa migogoro hiyo ni mikoa ya Manyara, Arusha na Morogoro ambako mapigano kati ya wakulima na wafugaji hutokea mara kwa mara.

Mikataba mibovu

Licha ya wananchi kupiga kelele kuhusu mikataba mibovu na usiri wao, bado suala hilo limekuwa kama barafu iliyowekwa juani.

Hadi sasa, hakuna kiongozi aliyeadhibiwa kwa kuiingiza nchi kwenye mikataba mibovu ambayo inapukutisha utajiri wa nchi.

Katika kuonesha kuwa mikataba hiyo ni tatizo, hivi karibuni Rais Magufuli aliagiza kufanyika mazungumzo ya kurekebisha mkataba wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Shehena ya Kontena Bandarini (TICTS), ili uwe na tija kwa Taifa. 

Hatua hiyo ya Rais ilikuja miezi mitano baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Juma Assad, kubaini Aprili mwaka huu kwamba kampuni hiyo imevunja mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo