Waziri abadili mfumo wa Bodi Chuo cha Utalii


Immaculate Ruzika

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameibadili Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utalii cha Taifa kuwa Bodi ya Utendaji.

Akizungumza juzi katika ziara yake chuoni hapo, alisema amebadili Bodi hiyo ili kuboresha utendaji wa chuo hicho.

“Kuwa Bodi ya Ushauri hakutoshi, sasa kuanzia leo naibadili  kuwa Bodi ya Utendaji ambayo licha ya kushauri, lakini pia itakuwa ikifanyia kazi yale inayoshauri kwa kuchukua hatua,” alisema.

Profesa Maghembe alisema ili kuboresha chuo hicho kuwa cha kisasa zaidi, itaundwa Bodi ya Taaluma itakayoshughulika na mambo ya kitaaluma, ili wanafunzi wanaomaliza chuoni hapo wawe wameiva sawasawa.

Alipendekeza chuo kuanzisha Stashahada ya Juu ili kuongeza ujuzi kwa wanafunzi wanaomaliza ikiwa ni mkakati wa kuifanya elimu hiyo kuwa ya kimataifa.

Waziri aliwataka wahadhiri wa chuo hicho kufanya kazi kwa bidii, ili chuo kiwe miongoni mwa vyuo bora Afrika.

Licha ya kusisitiza hayo, Maghembe aliwataka viongozi wa chuo  kudumisha uafi wa maeneo ya chuo, hususan jikoni na kwenye majokofu ya kuhifadhi chakula.

‘’Nimepita maeneo mbalimbali nimeona suala la usafi bado liko chini, hususan jikoni, hiki ni chuo cha kimataifa cha ukarimu, lazima kiwe safi maeneo yote,’’ alisema Waziri.

Aliongeza kuwa, chuo ni hazina kwa uchumi wa nchi na kuwa asilimia kubwa ya mapato ya Tanzania yanategemea sekta ya utalii.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo