Wazee ndio chanzo cha maambukizi ya Ukimwi – Waziri

Sharifa Marira, Dodoma

WAZEE  wametajwa kuwa na mtindo wa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na wasichana wadogo na kuwaambukiza Ukimwi hali inayochangia vijana hao kuusambaza  kwa vijana wenzao na hivyo kuongeza kasi ya maambukizi.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeeleza dhamira ya kuwekeza na kutekeleza sera na mipango ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi na vifo vya uzazi hasa kwa vijana wa kike ambao ndio wamebainika kuwa ni sehemu kubwa ya wenye maambukizi ya ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Hamis Kigwangallah alisema hayo mjini Dodoma jana alipozungumza kwenye semina ya siku mbili ya wabunge kuhusu changamoto za maambukizi ya Ukimwi, vifo vya uzazi na mimba za utotoni iliyoandaliwa na Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).

Dk. Kigwangallah alisema tahmini iliyofanywa imebainika kuwa watu wazima wengi ambao tayari wana wenza wao, hupenda kuanzisha uhusiano na vibinti vidogo ambavyo navyo vina wenza nao na matokeo yake, ugonjwa huo husambazwa kwa kasi kupitia mzunguko huo.

Alisema tafiti zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19 wanaoshiriki kwenye vitendo vya ngono wanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka, ingawa asilimia 40 ni vijana wa kike na asilimia 47 wa kiume ambao tayari wana ufahamu wa tatizo la Ukimwi.

Alisema Serikali imeamua kuwekeza zaidi kwenye kundi la vijana hasa mabinti wadogo ili kusambaza uelewa, lakini pia kuwaokoa na janga hilo la Ukimwi.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema  wabunge wana  jukumu la  kutumia fursa na wajibu wao wa kuishauri na kusimamia serikali na kuhakikisha inatekeleza mipango na mikakati yake iliyojiwekea katika kushughulikia matatizo hayo ya maambukizi ya ukimwi, vifo vya uzazi na mimba za utotoni.

Alisema wabunge ambao wanashiriki katika vikao vya bajeti, wahakikishe linapozungumziwa suala la afya ya uzazi, wanawake na vifo vya akinamama wakati wa kijifungua, mipango yake itekelezwe ipasavyo.

Naye Mkurugenzi wa Miradi na Mshauri wa Sera za Masuala ya Ukimwi SADC, Boemo Sekgoma aliishauri Serikali iangalie namna ya kutoa kipaumbele kwa masuala ya afya ya uzazi wa mpango kutokana na ukweli kwamba takribani asilimia 80 ya bajeti ya masuala hayo inatoka nje ya nchi na wakati mwingine haitoki kwa wakati.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo