Taarifa ya Lugumi yatua kwa Spika Ndugai


Sharifa Marira, Dodoma

Job Ndugai
RIPOTI ya utekelezaji wa ufungaji vifaa vya mashine za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi ulifanywa na kampuni ya Lugumi imetua mezani kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Ripoti hiyo ambayo iliagizwa na Bunge ndani ya miezi mitatu tangu Juni 30 iliwasilishwa jana kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projestus Rwegasira.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Katibu Mkuu huyo alifika PAC jana na kutoa taarifa kuhusu kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge.

Alisema kwa kuwa taarifa hiyo imemfikia Spika Ndugai ndiye atakayeiwasilisha kwenye Kamati hiyo kutokana na kwamba Bunge ndilo liliagiza awali.

Alibainisha kuwa baada ya Katibu Mkuu wa Wizara kutoa taarifa kwa Kamati juu ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge, PAC haijaijadili taarifa hiyo.

Juni 30 wakati wa kuahirishwa Bunge la Bajeti, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alisema Bunge liliiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi na pia PAC ifuatilie na kutoa taarifa kwenye taarifa yake ya mwaka.

Alisema Kamati ilibaini kuwa mradi huo unafanya kazi katika vituo 14 pekee kati ya 108 jambo ambalo lilikuwa linakwenda kinyume na mkataba.

Dk Tulia alisema kutokana na changamoto hiyo, PAC ilimtaarifu Spika ambaye aliwaruhusu kuunda kamati ndogo ambayo nayo ilifanya ukaguzi na kubaini upungufu.

Naibu Spika alisema baada ya kamati hiyo kupitia ilikubaliana kukabidhi taarifa hiyo kwa Spika ambaye naye aliona kuwa inastahili kuwasilishwa.

Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 117(17) Spika ataweka utaratibu wa kujadili taarifa ya Kamati na endapo kamati yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake, itaona kuna mambo ya utekelezaji, iyatoa taarifa maalumu kwa Waziri husika ili achukue hatua stahiki.

Katika sakata ilo, Lugumi Enterprises inadaiwa kupewa zabuni na Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo