Waziri Tamisemi atetea uchaguzi Meya Kinondoni


Fidelis Butahe

George Simbachawene
WAKATI leo Chadema ikitarajiwa kufungua kesi kuomba tafsiri ya Sheria za Serikali za Mitaa kwa madai kuwa ilikiukwa katika Uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni uliofanyika juzi, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, ameutetea akisema ulikuwa halali.

Waziri alitoa utetezi huo jana saa chache baada ya Meya huyo mpya aliyechaguliwa na madiwani wa CCM pekee, Benjamin Sitta kuanza kazi kwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) mjini Dodoma, huku wachambuzi wakisema uchaguzi huo ulifanyika kihuni.

Sitta alichaguliwa juzi na madiwani 18 wa CCM pekee, baada ya wa vyama vinavyounda Ukawa kususia uchaguzi huo katika kilichoelezwa kuwa ni kupinga mawaziri walioteuliwa na Rais kushiriki uchaguzi huo, huku baadhi ya madiwani wake wa viti maalumu, wakitakiwa kupiga kura kuchagua Meya wa Ubungo, badala ya Kinondoni.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuvunjwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo iligawanywa katika maeneo mawili ya kiutawala na kuzaa wilaya na manispaa mbili; Kinondoni na Kibamba. Uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Ubungo uliahirishwa.

Akizungumza na JAMBO LEO, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema kutokana na mchakato wa kuandaa utaratibu wa kufungua kesi kuwa mrefu, ilishindikana kuifungua jana, hivyo suala hilo litafanyika leo.

Akichambua jinsi Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) sura ya 288 ya mwaka 1982 na kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ya mwaka 2015 zilivyokiukwa, Makene alisema: “Kanuni zilizokiukwa ni ya 10 ambapo aliyeitisha uchaguzi aliamua kutumia kanuni ya 5(11)(12).”

“Kanuni ya 8 ambayo inahitaji taarifa ya kikao cha uchaguzi kiitishwe si chini ya siku saba au zisizozidi 21. Kama utakumbuka Mkurugenzi wa Kinondoni (Aron Kagulumjuli) aliitisha uchaguzi ndani ya saa kama 18 hivi.”

Alisema kanuni nyingine ni ya 9 inayozungumzia akidi za kikao, kwamba ili uchaguzi ufanyike ni lazima kikao kiwe na wajumbe 23, na kusisitiza kuwa uchaguzi huo ulifanyika huku ukumbi ukiwa na wajumbe 18 tu.

Akijibu hoja za baadhi ya madiwani na wabunge kutostahili kushiriki uchaguzi huo Simbachawene alisema: “Hakuna kitu kama hicho, sisi tumeweka mipaka ya Halmashauri na madiwani wanajulikana. Haiwezekani diwani apige kura sehemu isiyo yake. Nipo Dodoma sikuwa katika uchaguzi ila sidhani kama hili limetokea kweli.”

Alisema kwa kuwa yeye ni Waziri mwenye dhamana ya kusimamia halmashauri nchini, anasubiri kupelekewa malalamiko ili atoe ufafanuzi.

Sitta alisema: “Niko Dodoma kwenye kikao cha LAAC. Nilikuja huku jana (juzi) usiku baada ya uchaguzi pale Kinondoni.”

Alipoulizwa kama anahudhuria kikao hicho kama Meya, alisema: “Ndiyo unajua kuna mambo hapa ya Manispaa. Nipo kwa niaba ya Kinondoni. Ngoja nikimaliza kikao tutazungumza kwa kirefu nikueleze na mikakati yangu 15.”

Wachambuzi

Wakizungumzia uchaguzi huo kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema: “Huu ni ulaghai wa kisiasa. Hii inaonesha jinsi watu wanavyofanya mambo kwa ujanja ujanja. Idadi ya madiwani inajulikana wazi kwa kila chama…huu ni mwendelezo wa kutokuwa wakweli.”

Alisema ni ajabu kuona wabunge wasio madiwani wakihamishwa eneo moja kwenda lingine kupiga kura, “unaweza kusema CCM wamewazidi wenzao ujanja kama ambavyo wapinzani wanavyowazidi ujanja.”

Mhadhiri wa chuo hicho, Dk James Jesse alisema: ”Kama madai ya Ukawa na Chadema ni sahihi ni aibu kwa mustakabali wa Taifa letu. Kama tunataka nchi iwe na haki, usawa na demokrasia, lazima tuheshimu misingi ya haki.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema: “Umewahi kuona wapi Mkurugenzi wa Manispaa anaitisha uchaguzi bila kufuata mamlaka yake, yaani unaitisha kikao maalumu kwa ajili ya kufanya uchaguzi. Uchaguzi watu hufanya maandalizi na unatangazwa.

“Hivi umewahi kuona Mbunge wa Pemba (Profesa Makame Mbarawa-Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi), aliyeteuliwa na Rais anapiga kura kuchagua meya wa Kinondoni?”

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako waliapa wakati wa uchaguzi wa meya wa Ilala, lakini katika uchaguzi wa meya wa Kinondoni walipiga kura kumchagua Sitta na Naibu Meya, George Manyama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo