Kamati yaigomea Ofisi ya Makamu wa Rais


Joyce Kasiki, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, imetangaza kutoshirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kuwa imekuwa ikifanya mambo yake bila kuishirikisha.

Mambo hayo ni pamoja na kuendesha bomoabomoa ya nyumba za mabondeni na kufanya ziara kwenye maeneo ya migodi.

Mbali na hilo imegoma pia kujadili taarifa ya utupaji taka kwenye migodi iliyokuwa iwasilishwe na Ofisi hiyo, kwa madai kuwa kazi yao si kujadili taarifa wasiojua uhalisia wake.

Wakizungumza hapa jana, wajumbe wa Kamati hiyo walisema, Kamati yao ni nyeti hivyo inapaswa kutengewa fedha za kutosha, ili itembelee maeneo mbali mbali yakiwamo ya migodi ili  kujionea utupaji taka na bomoabomoa mabondeni jambo ambalo walisema Ofisi hiyo haiipi ushirikiano.  

Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) alisema inasikitisha kuona Serikali yenye kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu, inabana matumizi hadi kwa wabunge ambao wanafanya kazi zake.

"Si kwamba sisi wabunge tunakubaliana  na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, lakini haiwezekani wabunge walio kwenye Kamati nyeti ya mazingira, wananyimwa fedha za kutembelea maeneo ambayo yanaonekana kuwa na mkanganyiko kwa nia ya kuishauri Serikali,” alisema.

"Hii Kamati si ya kujadili taarifa tu kwa lengo la kuishauri Serikali bila kufika sehemu husika ili kujiridhisha," alisema Mbunge huyo.

Mbunge wa Viti Maalumu,Thauhida Nyimbo (CCM) alisema wabunge hawapo kwa ajili ya kufanya kazi za Serikali,  wala kufurahisha mawaziri na timu zao, bali kusimamia  Serikali  kwa maslahi  ya wananchi.

“Hivi hapa Naibu Waziri na timu yako mnatuletea hii taarifa   tujadili kitu gani au nyie Wizara hamjui wajibu wenu? Hivi kweli mnadhani sisi hapa ni wasaidizi wenu au tunafanya kazi za Serikali? Kazi yetu ni kuishauri Serikali na si kufanya kazi za Serikali,” alisema.

Mbunge  wa Konde, Khatibu Haji Kombo (CUF) alisema kama Kamati haitakuwa karibu na Wizara, kwa maana ya kufanya ziara katika maeneo yenye migogoro ni bora isifanye jambo lolote na Wizara hiyo.

Alisema inakuwaje masuala muhimu kama sumu za taka katika maeneo ya migodi na sehemu za bomoabomoa mabondeni, wabunge wa Kamati husika wasiende kujionea kinachofanyika  na kuhoji wananchi ili kupata picha kamili.

Mbunge wa Moshi Mjini, Anthony Komu (Chadema) aliunga mkono kukataliwa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, kwa madai kuwa wakiijadili watakuwa hawatendei haki wananchi.


Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima (CCM) alisema ripoti hiyo haioneshi malengo ambayo yamefikiwa na Serikali na pia hawana uelewa mpana kuhusu mazingira ya nchi yao, hivyo wanahitaji kufika maeneo husika ndipo warudi kujadili ripoti hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina akijibu, alisema Wizara imeonewa kwani si jukumu lake kuratibu ziara za Kamati na wala si jukumu la Ofisi ya Makamu wa Rais bali ni Kamati kusema kama inataka ziara.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo