Shule Shinyanga yavunja rekodi


Celina Mathew

Dk. Charles Msonde
SERIKALI imetangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba uliofanyika Septemba 7 na 8 huku shule ya msingi ya Kwema ya mkoani Shinyanga ikiongoza kwa kutoa watahiniwa saba bora kitaifa kati ya Kumi Bora na kuongoza kitaifa.

Akitangaza matokeo hayo jana Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk Charles Msonde alisema watahiniwa 555,291 kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata alama 100 au zaidi ya alama 250.

Alisema idadi hiyo ya watahimiwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36 na kwamba kati yao, wasichana ni 283,751 sawa na asilimia 67.59 na wavulana ni 271,540 sawa na asilimia 73.50 ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo watahiniwa walikuwa asilimia 67.84 hivyo ongezeko la asilimia 2.52 ya ufaulu.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa ufaulu katika masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii umepanda kwa asilimia kati ya 4.06 na 14.76 ikilinganishwa na mwaka jana.

Kwa upande wa masomo ya Kiswahili, Hisabati na Kiingereza, Dk Msonde alisema ufaulu umeshuka kwa kati ya asilimia 0.39 na 12.51 ikilinganishwa na mwaka jana.

Alisema watahiniwa wamefaulu zaidi Kiswahili unaofikia asilimia 76.81 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini zaidi ni Kiingereza ambayo ni asilimia 36.05.

Wahitimu 10 bora

Alitaja wanafunzi kumi bora kuwa ni Japhet Stephano (Kwema, Shinyanga), Jamal Athuman, Enock Bundala, Justina Gerald (Tusiime, Dar), Shabani Mavunde (Tusiime), Jacob Wagine (Kwema), Isaac Issac (Kwema), Daniel Kitundu (Kwema), Benjamin Shabu (Kwema) na Azad Ayatullah wa (Kaizirege, Kagera).

Wasichana 10 bora

Kwa wasichana 10 bora aliyeongoza ni Justina Gerald, akifuatiwa na Danielle Onditi wote wa Tusiime, huku wa tatu akiwa ni Linda Mtapima (Kaizirege).

Wengine ni Cecilia Kenene (Mugini, Mwanza), Magdalena Deogratius (Rocked Hill, Shinyanga), Asnath Lemanya (Tusiime), Fatuma Singili (Rocken Hill).

Pia Ashura Makoba (Kaizirege), Rachel Ntitu (Fountain Of Joy, Dar) na Irene Mwijage (Atlas, Dar).

Wavulana 10 bora

Wavulana 10 bora ni Japheth Stephano (Kwema), Jamal (Kwema), Enock Bundala (Kwema), Shabani Mavunde (Tusiime), Jacob Wagine (Kwema), Isaac Issac (Kwema), Daniel Katundu (Kwema), Benjamin (Kwema), Azad Ayatullah (Kaizirege) na Beneth Hango (Kwema).

Shule 10 bora

Shule zilizo kwenye kundi la 10 bora kitaifa ni Kwema, Rocken Hill, Mugini, Fountain of Joy, Tusiime, Mudio Islamic (Kilimanjaro), Atlas, St. Achileus (Kagera), Gift Skillfull (Dar) na Carmel ya Morogoro.

Shule 10 za mwisho

Shule 10 zilizoshika mkia ni Mgata (Morogoro), Kitengu (Morogoro), Lumba Chini (Morogoro), Zege (Tanga), Kilole (Tanga), Magunga (Morogoro), Nchinila (Manyara), Mwabalebi (Simiyu), Ilorienito (Arusha) na Chohero ya Morogoro.

Mikoa 10 bora

Dk Msonde aliitaja mikoa 10 iliyiofanya vizuri kitaifa kuwa ni Geita, Katavi, Iringa, Dar es Salaam, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Njombe na Tabora.

Halmashauri 10 bora

Halmashauri zilzofanya vizuri kitaifa alizitaja kuwa ni Mpanda (Katavi), Geita Mjini (Geita), Arusha Mjini, Mafinga Mjini (Iringa), Chato (Geita), Mwanza Mjini, Moshi Mjini (Kilimanjaro), Makambako Mjini (Njombe), Ilemela (Mwanza) na Hai (Kilimanjaro).

Hata hivyo, Dk Msonde alisema Baraza hilo liliwafutia mitihani wanafunzi 238 waliobainika kufanya udanganyifu kwa mujibu wa kifungu 32(2)(b) cha kanuni za mitihani.

Aidha, Baraza lilishauri mamlaka husika kuwachukulia hatua waliohusika kwa namna moja au nyingine kusababisha udanganyifu huo kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo