Quality Group kuunganisha matrekta nchini



 
Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Quality Group Limited (QGL) imeingia ubia na kampuni ya kimataifa ya India iitwayo International Tractors Limited (Sonalika) kwa ajili ya kuanza kuunganisha matrekta ya Sonalika nchini.

Akizungumza jana Dar es Salaam, kwenye hafla ya kusaini  makubaliano hayo, Ofisa Uendeshaji Mkuu wa QGL, Constantinos Vasileiadis alisema makubaliano hayo yanalenga kuinua sekta ya kilimo kwa kuunganisha matrekta nchini na kupunguza gharama za ununuzi.

“Tumesaini makubaliano na International Tractors Ltd ili kuanza kuunganisha matrekta ya Sonalika nchini, ikiwa ni juhudi za kuchochea maendeleo ya viwanda ambavyo vitasababisha kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema.

“Pia, uunganishaji huo wa matrekta utapunguza gharama   ambazo wakulima walikuwa wakizipata katika ununuzi wa nyenzo hizo za kilimo.

“Zitauzwa kwa gharama nafuu zaidi, hivyo kuwa kichocheo cha wakulima kuondokana na jembe la mkono,” alisema Vasileiadis.

Aidha, Vasileiadis alisema mara uundaji huo utakapoanza baada ya taratibu zote kukamilika, kiwanda kinatarajiwa kuwa Morogoro na kitakuwa kikiunganisha matrekta 1,000 kwa mwaka na kupunguza pengo la mahitaji ya nyenzo hizo.

“Kwa sasa kuna mahitaji ya matrekta 5,000 kwa mwaka, lakini yanayokuja nchini ni 800 tu. Uunganishaji utakapoanza tutaunganisha matrekta 1,000 na kufikia 1,800 na kupunguza kwa kiasi pengo hilo.

“Matrekta hayo yatakuwa na nguvu tofauti kulingana na uwezo wa mkulima kiuchumi. Tutaunganisha matrekta ya kuanzia nguvufarasi 20 hadi 110. Na zitakuwa zikiuzwa kwa bei ndogo kulingana na ukubwa wa nguvu ya trekta,” alisema Vasileiadis.

Rais wa International Tractors Ltd, Gaurav Saxena alisema  kampuni hiyo imeingia ubia na QGL kwani wamekuwa wakifanya nao biashara kwa muda mrefu na kuunga mkono juhudi za kuendeleza uchumi wa viwanda.

“Tanzania ni nchi ambayo uchumi wake unategemea kilimo, lakini wananchi wake wengi wamekuwa wakitegemea kilimo cha jembe la mkono. Sasa ubia wetu na Quality Group utamsaidia mkulima moja kwa moja, kwani tutakuwa tukiunganisha matrekta ya bei nafuu kulingana na mahitaji ya mkulima.

“Pia, utasaidia kuchochea juhudi za nchi kuelekea katika uchumi wa kati na viwanda, kama ambavyo Rais John Magufuli anavyotaka. Tumefurahi zaidi kwani tutawasaidia wakulima wa madaraja yote kwa kuwapa bidhaa bora zenye ufanisi mkubwa,” alisema Saxena.

Meneja Masoko wa QGL, Timothy Shuma alisema kwa sasa kampuni ipo katika mazungumzo na Serikali kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupata kibali cha kuanzisha kiwanda hicho na kuanza uzalishaji mara moja Morogoro.

“Tupo katika mazungumzo na Serikali kupata kibali cha kujenga kiwanda Morogoro. Kinatarajiwa kugharimu Sh bilioni 50 hadi Sh bilioni 100. Pia, kitazalisha nafasi za ajira zaidi ya 5,000,” alisema Shuma. 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo