JK aahidi kutatua matatizo UDSM


Hussein Ndubikile

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Rais mstaafu Jakaya Kiwete, ameahidi kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi chuoni hapo likiwamo suala la mikopo kwa kuwasiliana na Serikali kuhakikisha changamoto hiyo, elimu na ujenzi wa mabweni.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini katika maadhimisho ya miaka 55 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo.

Alisema baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuongoza chuo hicho, aliwasiliana na viongozi wa chuo na Serikali ili kuona miundombinu inaimarishwa huku akisisitiza kuwa mazungumzo hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mabweni unaoendelea chuoni hapo.

"Naahidi nitaendelea kufanya kazi na Baraza la Chuo, Serikali na wadau kutafuta njia ya kutatua matatizo ya mikopo, mahali pa kulala wanafunzi na miundombinu mingine, yote ni kukifanya kiendelee kuwa na hadhi yake," alisema.

Dk Kikwete alisema jamii inatakiwa kutambua mchango wa chuo hicho katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuzalisha viongozi wa Serikali, wachumi, wakuu wa idara taasisi za umma na binafsi na wanasheria na kuongeza kuwa utafiti wa wanafunzi wa chuo hicho umesaidia kuleta matokeo chanya kwenye jamii.

Alitaka viongozi na wanafunzi wa Udsm kuendeleza juhudi ili kiendelee kuongoza huku vingine vikifuatia ambapo pia alimpongeza Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere kwa mchango mkubwa uliofanikisha kuanzishwa chuo hicho.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, alimpongeza Dk Kikwete kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu hasa ujenzi wa mabweni unaoendelea na kusisitiza kuwa chuo hicho ni miongoni mwa vyuo bora kwenye ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alifafanua sababu zinazofanya kiwe bora ndani na nje ya nchi kuwa ni mchango wake wa kuzalisha marais wa nchi, viongozi na bado kinakabiliwa na changamoto za vitendea kazi vya maabara, ukosefu wa wafanyakazi hali inayosababisha utekelezaji wa shughuli chuoni hapo kushindwa kufanyika ipasavyo.

Mhadhiri mwalikwa ambaye pia ni mteule wa mkuu wa chuo, Profesa Tade Aina alivishauri vyuo vikuu vya Afrika kuendeleza misingi, mipango na malengo yaliyofanya vianzishwe ikiwamo kutoa viongozi waliopigania uhuru wa nchi zao.

Aliwataka viongozi wa Afrika kuendeleza mawazo ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiswahili ambacho kitatumiwa na wasomi wa ndani na nje kujifunza lugha hiyo hali itakayochangia kuondoa mawazo na fikra za kikoloni.

Alishauri viongozi wa chuo kuboresha ufundishaji kwa kutilia mkazo ufanyaji utafiti mbalimbali utakaotoa wahitimu bora watakaoleta tija.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo