Shahidi: Gwajima alipelekewa bastola wodini


Grace Gurisha

Josephat Gwajima
MPELELEZI wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sajini Abogasti ameieleza Mahakama kuwa wasaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima walimpelekea bastola saa nane usiku akiwa hospitali ya TMJ alikolazwa baada ya kuanguka Polisi akihojiwa.

Sajini Abogasti alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi dhidi ya Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na tuhuma za kushindwa kuhifadhi silaha sehemu salama.

Shahidi huyo alitaja wasaidizi hao kuwa ni Yekonia Bihagaze, George Mzava na Geofrey Milulu, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha sheria kwa sababu kwa hali ya kawaida mgonjwa hapalekewi silaha.

Alidai wasaidizi hao walikutwa na begi ambalo ndani lilikuwa na silaha na vitu vingine, baada ya askari kulifungua wakihisi kuwapo jambo linaloendelea.

Alidai kuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni alimuunganisha na Mkuu wa Kituo cha Kawe, Pamphil ambaye alimkabidhi begi lenye bastola namba CAT 5802, risasi tatu kwenye magazine, CD mbili, risasi 17 za SMG, kitabu cha umiliki silaha, nguo ya ndani na hati ya kusafiria ya Mchungaji huyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro, alimtaka shahidi wa upande wa mashitaka kuionesha Mahakama kitabu cha umiliki wa silaha ambapo shahidi huyo alikitafuta zaidi ya dakika mbili bila mafanikio.

Hata hivyo, alidai kitabu cha umiliki wa silaha na cha hundi alimshampa Gwajima.

Alidai kuwa baada ya kukabidhiwa begi hilo kwenye kituo cha Polisi Oysterbay alianza upelelezi na kubaini kuwa Machi 25 mwaka jana, Gwajima alikwenda Arusha kwenye mkutano wa maaskofu na washitakiwa wenzake.

“Machi 26 mwaka jana, Gwajima aliambiwa anaihitajika Polisi Dar es Salaam, Machi 27 alifika na kuacha silaha yake mikononi mwa Bihagaze, Mzava na Milulu ambao walikaa nayo kwa siku mbili kitu ambacho ni kinyume cha utaratibu,” alidai shahidi huyo.

Alidai pia kwamba Gwajima aliitwa polisi kwa tuhuma za kumdhihaki Askofu Mkuu wa Jimbvo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kadinali Pengo.

Sajini Abogasti alidai mahojiano ya polisi na Gwajima yaliisha baada ya Gwajima kupata maradhi ya ghafla ambapo aliondolewa kituoni hapo na kupelekwa kwa mara ya kwanza hospitali ya Temeke, kisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwishowe TMJ kutokana na hali yake ilivyokuwa.

Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala alimhoji, shahidi huyo kuwa Gwajima alipofika kituo kikuu cha Polisi, upelelezi wake ulibaini kuwa maungoni alikuwa na silaha.

Akijibu hoja hiyo, Sajini Abogasti aligundua kuwa Gwajima alishaitekeleza na kuwa yeye si aliyemfundisha Gwajima taratibu za kumiliki silaha. Kesi iliahirishwa hadi Novemba 24.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo