Agizo la JPM kwa wamachinga layeyusha mabilioni Dar


Salha Mohamed

Wamachinga Kariakoo
SERIKALI imepoteza zaidi ya Sh bilioni 100 kutokana na uwepo wa wamachinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa ambao hawalipi kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hali iliyosababisha kutoa siku 14 waondoke maeneo hayo.

Hasara hiyo ya Septemba pekee, imetajwa kutokea baada ya agizo la Rais John Magufuli lililotaka wamachinga wasibughudhiwe.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema jana kuwa hasara hiyo inatokana na wamachinga kushirikiana na wanaohifadhi bidhaa kwenye maghala na kufunga maduka yao hivyo kutolipa kodi akisema Ilala peke yake imeingiza hasara ya zaidi ya Sh bilioni 54.

 “Sasa wamachinga wameanza kutumika na waliokuwa na mizigo kwenye maghala na mwishowe tumejikuta mapato yamepungua kwa TRA mkoani kwetu,” alisema.

Alisema wamachinga hao wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu za kuuza bidhaa nje ya maduka ya wafanyabiashara wanaostahili kulipa kodi.

Alisema kupungua kwa mapato hayo, kunatokana na wamachinga hao kuchukua bidhaa na kuingia mtaani kisha kuziuza kwa bei wanayotaka, huku akibainisha kwamba kwa hali hiyo, uchumi wa nchi hauwezi kujengeka.

“Nawapa siku 14 wakuu wangu wa wilaya kuwa mmachinga ambaye hana sehemu ya kufanyia biashara ampe, kwani kila wilaya imetengewa eneo la wafanyabiashara.

“Nawaomba wamachinga wale ambao wana maeneo yao warudi kwenye maeneo yao, ambao hawana wawaone wakuu wa wilaya au wakurugenzi wao watawapangia maeneo husika,” alisema.

Alitoa rai kwa wakuu wa wilaya wake kuhakikisha kila mmachinga anakwenda sehemu stahiki, kwani zipo za masoko ambazo ziko wazi lakini hawafanyii biashara kwa kukimbilia barabarani.

Alifafanua, kuwa kwa sasa kila eneo wamachinga wapo huku wakinyima watu wengine haki ya kutumia barabara hizo, kwa kupanga bidhaa zao.

Alisema maeneo ya barabarani ni ya hatari, hivyo wasingependa kuona wamachinga kwenye maeneo hayo na kutoa mwito kwamba Serikali ilijenga barabara si kwa matumizi ya kupanga viatu na nguo.

 “Wafanyabiashara wenye maduka yao wanashindwa kufanya biashara vizuri kwa sababu mbele ya duka kuna bidhaa zinazotandikwa chini,” alisema.

Makonda aliongeza kuwa wananchi wanaofanya ununuzi katika maeneo hayo hulalamika uhalifu sababu mazingira hayaruhusu kukamata mwizi.

Aliongeza kuwa mbali na kutolipa kodi lakini wamachinga wamekuwa wakichafua mazingira kwa kuzalisha uchafu na kuuacha huku wananchi wa kawaida wakishindwa kutembea vema barabarani.

Alisema si vema itumike nguvu kuwaondoa huku akiwatakia kila la heri katika utafutaji wao wa kipato usio na kero kwa watu wengine.

“Maeneo ya barabara za mwendo wa haraka naomba wapishe…Kariakoo yote tulisema barabara ya magari yaendayo haraka ipitike kirahisi, nako wamevamia hadi barabara ya Ikulu na sehemu zingine za vituo vya daladala wameviua na kupanga bidhaa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo