Umeya Kinondoni, Ubungo vurugu tupu


Waandishi Wetu

UCHAGUZI wa mameya katika manispaa za Kinondoni na Ubungo jana ulizua mvutano kati ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa kuhusu uhalali wa baadhi ya wajumbe kupiga kura, huku Benjamin Sitta aliyechaguliwa na madiwani wa CCM pekee, akitangazwa kuwa Meya mpya wa Manispaa ya Kinondoni.

Katika mvutano huo, madiwani wa Ukawa Kinondoni walisusia uchaguzi huo huku ule wa manispaa ya Ubungo ukiahirishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa madiwani wa Chadema ambao ndio wengi kuliko wa CCM, kupinga baadhi ya madiwani wao wa Ubungo kutakiwa kupiga kura Kinondoni, huku wale wa Kinondoni kuhamishiwa Ubungo.

Uchaguzi huo ulipangwa baada ya kuvunjwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo iligawanywa katika maeneo mawili ya kiutawala na kuzaa wilaya na manispaa mbili; Kinondoni na Kibamba.

Mvutano katika chaguzi hizo ulianza kuonekana tangu juzi baada ya vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kudai kuna ‘mkakati’ wa kuongezwa kwa wajumbe ili CCM iibuke na ushindi.

Wakati Ukawa ikipinga wabunge wake wa viti maalum, Susan Lyimo (Chadema) na Salma Mwasa (CUF) kutakiwa kushiriki uchaguzi wa meya wa Ubungo badala ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema wabunge hao wote wanaishi Ubungo, hivyo walipaswa kushiriki uchaguzi huo.

Ukawa pia walipinga kitendo cha Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuongezwa kuwa wajumbe halali wa uchaguzi wa meya wa Kinondoni, kwa maelezo kuwa ni kinyume na sheria za Serikali za Mitaa.

Sakata hilo lilisababisha Chadema kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kusudio la kwenda mahakamani kupinga chaguzi hizo wakibainisha kuwa hali hiyo imeamsha upya mkakati wao wa operesheni Ukuta.

Wakati Ukawa wakijipanga kwenda mahakamani, Kagulumjuli aliwatangazia vita, akieleza kuwa iwapo madiwani wa Ukawa watashindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo vya Baraza la Madiwani, watakuwa wamejiondoa kwenye nafasi hizo na kwa mamlaka aliyonayo ataitisha uchaguzi mwingine kwenye kata zao.

Hali ilivyokuwa Kinondoni

Uchaguzi huo ulipangwa kuanza saa 2:30 asubuhi lakini mbali na Ukawa kuususia, waandishi wa habari nao walibaguliwa kwa kuruhusiwa wachache kutoka vyombo vya habari vya Serikali, chama tawala, Clouds televisheni na Star televisheni.

Kuhusu madiwani na wabunge wa viti maalum wa Ukawa kuondolewa katika uchaguzi kwa madai kuwa si wajumbe halali wa kikao, huku wale wa CCM wasio halali wakiruhusiwa kushiriki alisema ni uhuni uliopitiliza.

“Wamemkata Lyimo na Mwasa. Sheria inasema wajumbe halali wa vikao vya halmashauri ni wabunge wa viti maalum ambao mchakato wao umeanzia katika halmashauri na hao waliowakata michakato yao imeanzia Kawe na Kinondoni. Ni wajumbe halali na ndio maana waliingia katika vikao vilivyopita,” alisema.

Alidai kuwa madiwani wa viti maalumu wa Ukawa pia wamekatwa kushiriki uchaguzi, kufafanua kwamba idadi ya madiwani hao katika halmashauri husika hutokana na idadi ya kata ambayo chama kimeshinda katika halmashauri hizo.

Alibainisha kuwa kutokana na idadi ya kata ambazo Ukawa wameshinda katikamajimbo ya Kawe na Kinondoni, walipaswa kuwa na madiwani saba wa viti maalum.

“Baada ya kupatikana kwa halmashauri mbili mkurugenzi wa kinondoni amechukua hatua ya kukata madiwani wawili wa viti maalum wakati Tume ya Taifa ya Uhaguzi (NEC) ndio ina mamlaka ya madiwani na wabunge,” alisema.

Kuhusu wateule wa Rais walioshiriki uchaguzi huo alisema, “Ili aweze kuingia katika halmashauri husika lazima awe mkazi wa halmashauri hiyo. Yupo Dk Tulia, Ndalichako ambaye ni mpya na alishiriki uchaguzi wa meya wa Ilala ila leo kaletwa Kinondoni.”

Alisisitiza, “wateule wa rais hawawezi kuingia zaidi ya watatu katika halmashauri moja, ila ndani kwenye uchaguzi (wa jana) wapowanne. Huu ni uhuni na kama amewatuma (Rais John Magufuli) sawa, ila tutaenda kupambana mahakamani ili tupate tafsiri ya sheria.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, aliponda uchaguzi huo na kubainisha kuwa ni mwendelezo wa Serikali ya Awamu ya Tano kuminya demokrasia.

“Serikali hii haizingatii demokrasia wala kufuata sheria na katiba na polisi wamekuwa mawakala wa CCM…, huyu meya wao ‘magumashi’ (Sitta) watakayefikiria wamempata nina imani hana baraka za wananchi na Mungu na sisi hatuna sababu za kumpa baraka.”

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai aliponda kitendo cha kuzuiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari kuripoti uchaguzi huo, kuruhusiwa vile vya Serikali na CCM, kukifananisha kitendo hicho na uhuni uliopitiliza. “Ndani (katika ukumbi) kuna askari wengi wenye sare na wasio na sare.

Rais Magufuli kwa utaratibu huu wa kuua demokrasia aliouanzisha katika utawala wake ataliletea Taifa hili maafa makubwa,” alisema Mbowe.

Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji, alisema kitendo kilichotokea katika chaguzi hizo kitaamsha upya mkakati wa operesheni Ukuta ambayo Septemba 30 mwaka huu, kilitangaza itafanywa kimya kimya.

Operesheni hiyo ambayo awali ilipangwa kuandamana na mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima inalenga kila kinachoelezwa kuwa ni kupinga maamuzi yanayofanywa na Serikali bila kuzingatia sheria na Katiba ya nchi, likiwemo la kuzuia mikutano ya hadhara.

Mashinji alilalamikia kitendo cha madiwani kupewa barua za kushiriki uchaguzi huo juzi saa mbili usiku na kubainisha kuwa watakwenda mahakamani kupinga uvunjwaji wa sheria na kanuni zinazoweka haki ya madiwani kuchagua viongozi wao katika Halmashauri husika.

Meya wa CCM alichaguliwaje?

Sitta aliibuka mshindi kwa kupata kura 18, huku Naibu Meya akichaguliwa George Manyama naye akishinda kwa idadi hiyo hiyo ya kura. Awali, Ukawa ilikuwa na wajumbe 17 na CCM wakiwa 16 lakini baada ya chama hicho tawala kuongeza wajumbe kwa hoja zilizotolewa na Kagurumjuli, CCM kilikuwa na wajumbe 18 huku Ukawa wakibaki 17.

Katika maelezo yake ndani ya uchaguzi huo ambayo JAMBO LEO imeyanasa, Kagulumjuli alisema taarifa za uchaguzi huo zilitolewa mapema na madiwani wote walipewa taarifa.

“Wajumbe wote walipata barua ya wito na kuzipokea kupitia “dispatch” lakini baadhi yao, wamefika na kugoma kuingia ndani. “Kukaa kwao nje hakutuzuii kuendelea na uchaguzi kwa sababu taratibu zote zimefuatwa,” Mkurugenzi huyo alieleza.

Awajibu Ukawa

Akijibu suala la Lyimo na Mwasa, alisema Lyimo si mkazi wa Kinondoni anaishi eneo la Chuo Kikuu lililopo Ubungo, hivyo anapaswa kushiriki kwenye vikao vya baraza la madiwani kwenye wilaya hiyo mpya.

Kuhusu Mwasa alisema ni mkazi wa Kimara na kwa sababu hiyo alipaswa kushiriki vikao hivyo kupitia manispaa ya Ubungo.

Katika maelezo yake Kagurumjuli, alisema wajumbe ambao ni wateule wa rais wabunge hao wanachaguliwa na rais kwa majukumu maalum na hawana mchakato kwani mchakato wao unafanywa na rais mwenyewe.

Mkurugenzi huyo aliagiza kusomwa barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, ikifafanua kuhusu makazi ya Profesa Ndalichako kuwa ni mkazi wa Kinodnoni ambaye kabla ya uchaguzi huo alikula kiapo cha kuwa diwani wa manispaa hiyo.

Hali Ubungo ilikuaje?

Katika manispaa ya Ubungo, mgombea umeya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob aliwaongoza wenzake kugomea uchaguzi ulioitishwa na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, John Kayombo.

Katika maelezo yake, Jacob alisema taarifa za mkutano wa uchaguzi wa meya walipewa juzi saa sita usiku, huku kukiwa na sintofahamu ya idadi ya wajumbe.

Aliwataja madiwani waliotolewa Ubungo kupelekwa Kinondoni na kutolewa Kinondoni kupelekwa Ubungo ili kuiongezea CCM kura kuwa ni Lyimo, diwani wa Mabwepande (CUF), Leyla Madibi.

Wengine ni diwani wa Saranga (CCM) Florence Masunga aliyetolewa Ubungo kupelekwa Kinondoni pamoja na Dk Tulia ambaye ni mkazi wa Kibamba, lakini kapiga kura Kinondoni.

Naye mbunge wa Kibamba, John Mnyika alisema kilichotokea ni maelekezo ya Rais John Magufuli kuhakikisha CCM kinashinda Kinondoni.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Husein Ndubikile, Suleiman Msuya na Abraham Ntambara
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo