Uhalifu wapangwa kuitikisa Serikali


*Waendana na matukio ya kupora silaha, kuua
*Polisi yasema iko imara inaendelea kupambana

Mwandishi Wetu

Rais John Magufuli
LICHA ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi kukabili uhalifu nchini, taarifa za uhakika kutoka Jeshi hilo zinaonesha kwamba matukio ya uhalifu unaombatana na uporaji wa silaha hufanyika kwa kupangwa na watu wenye malengo ya kufanikisha mambo yao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi hilo, watu hao hupanga na kutekeleza matukio hayo wakilenga kuitikisa nchi hata Serikali ili kufanikisha mambo wanayoyataka kwa maslahi yao.

Habari zilizoifikia JAMBO LEO zinaeleza kwamba majambazi wanaopora silaha hizo, hupanga kuzitumia kwenye matukio yanayolenga kuvuruga amani na utulivu nchini, ili kujijengea uhalali wa kutekeleza mipango yao inayokwenda kinyume na ile ya Serikali na Taifa kwa jumla.

Taarifa zinaonesha kuwa tangu Januari mwaka juzi hadi jana matukio zaidi ya 10 ya ujambazi yaliyoambatana na uporaji wa silaha na mali na watu kujeruhiwa pamoja na vifo kutokea yaliripotiwa.

Hata hivyo, baada ya matukio hayo, polisi kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa taarifa ya kukamata silaha hizo.

“Haya si matukio ya kawaida, ingawa watu wakiona yanatokea wanadhani kuwa ni ujambazi. Kuna watu wana mambo yao ili nchi ionekane haijatulia,” alieleza mmoja wa maofisa wa Jeshi hilo mwenye cheo cha Inspekta.

“Tuna kazi kubwa, lakini tunapambana kwa nguvu zote kuhakikisha matukio hayo yanakoma. Haya matukio ni zaidi ya watu wanavyoyafikiria.”

Kuhusu matukio ambayo askari walipoteza maisha, mtoa taarifa huyo alisema ni jambo linalohuzunisha kwa kiasi kikubwa, lakini inatokea katika mapambano yenye lengo la kukabili uhalifu huo.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu hakukiri wala kukanusha, lakini akasema huenda taarifa hizo ni maoni ya watu ambayo mwandishi wa habari hizi ameyasikia.

“Matukio ya ujambazi yanayotokea ndiyo hayo ambayo mnayasikia polisi wakiyatolea ufafanuzi…ujambazi tunashughulika nao miaka nenda rudi na wala si ajabu Polisi kukabiliana na wahalifu na majambazi,” alisema Mangu.

Aliongeza: “Tunapokamata majambazi tunatoa taarifa na kwa sababu hilo unalonieleza huenda ikawa mtazamo ya mtu, siwezi kuchangia mengi kuhusu jambo hilo.”

Katika maelezo yake, mpashaji habari wa JAMBO LEO alisema watu hao wanalenga kuandaa kikundi kitakachokuwa kikishiriki matukio ovu na kwamba polisi wanalijua hilo na kwamba kundi hilo haliwezi kufika kokote.

“Kaka we acha tu watu wakiona haya mambo (ujambazi) kila mmoja anasema lake, lakini ukweli ni kwamba kuna kitu nyuma ya haya mambo,” alisema.

Mwananchi ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema anaamini kasi aliyonayo Rais John Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo haifurahishi baadhi ya watu waliodhani angeshindwa.

“Haya mambo yanawezekana kweli yakawa yanahusishwa na siasa, kwa sababu kuna watu aliokuwa akipambana nao kwenye uchaguzi walidhani atashindwa kukabiliana na uovu, lakini kasi hii inawatisha wanajaribu kumvuta shati,” alisema.

Matukio

Septemba 5 katika tukio la Vikindu mkoani Pwani ambako polisi walijibizana risasi na majambazi na askari mmoja kuuawa, walikamata majambazi watatu waliohusika na tukio hilo ambao waliwapeleka polisi eneo la Mbezi Chini kwenye nyumba waliyokuwa wamekodi na askari kufanya upekuzi na walifanikiwa kupata silaha, zikiwamo bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu vingine.

Pia walikuta redio za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea mbali tatu, pingu za plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi wa kukatia vyuma, mtaimbo, risasi baridi za kutishia 37, kasha la kusafirishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine ya kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.

Julai 12, watu walioaminika kuwa majambazi walivamia kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam kuua askari wanne na watatu wengine na kisha kupora silaha zinazosadikiwa kuwa ni zaidi ya 20.
Septemba mbili, majambazi walivamia na kuua mlinzi wa Chuo cha Sebastian Kolowa (Secomu) na kumpora silaha aliyokuwa nayo.

Tukio hili lilishuhudiwa pia mmoja wa majambazi hao akipigwa risasi na wenzake akihofiwa kuvujisha siri zao, baada ya pikipiki aliyokuwa akitumia, kugoma kuwaka baada ya kukamilisha uhalifu huo.

Januari 21 mwaka jana, majambazi yaliojihami kwa silaha walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Rufiji mkoani Pwani na kuua askari wawili na kupora silaha zilizokuwa kituoni hapo.

Silaha zilizoporwa ni SMG mbili, SAR mbili, shotgun moja, mabomu ya kutoa machozi na risasi 60 za SMG.

Siku sita baadaye, Januari 27, mkoani Tanga watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, walivamia na kujeruhi askari wakiwa doria ya pikipiki na kuwanyang’anya silaha mbili aina ya SMG.

Februari 3 mwaka jana, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, walivamia na kuvunja stoo ya Kituo Kidogo cha Polisi Mngeta, Kilombero, Morogoro na kuiba SMG ikiwa na risasi 30, pia waliiba jenereta, redio, viti, betri ya gari na spika ya redio.

Machi 30 mwaka jana, askari wawili waliuawa na mmoja kujeruhiwa na majambazi Kongowe, Dar es Salaam na kuporwa SMG mbili.

Mei 29 mwaka jana, Dar es Salaam, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, walivamia lindo askari wa Kikosi cha Tazara, Dar es Salaam na kupora SMG.

Juni 12 mwaka juzi, majambazi wanaokadiriwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba Kimanzishana, Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo wawili na kupora bunduki tano na risasi 60.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo