Bomoabomoa yakumba nyumba 150 Dar es Salaam


* Kaya zaidi ya 450 zahaha mahali pa kuishi
* Mbomoaji asema ni wavamizi wasio na haki

Dotto Mwaibale

Baadhi ya wakazi wa Madale
KAYA zaidi ya 450 hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao zaidi ya 150 kubomolewa Tegeta A, kata ya Goba, Dar es Salaam kwa madai ya kujengwa eneo lisilo lao.

Ubomoaji huo, ulifanyika jana ukisimamiwa na askari wa Jeshi la Polisi chini ya kampuni ya Udali ya Yono Aution Mart, ambao hata hivyo umepingwa na wananchi hao wakidai eneo hilo ni lao na wapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Ubomoaji wa nyumba hizo ulisimamiwa na polisi zaidi ya 15 wenye silaha za moto na mabomu ya machozi huku wakiwa katika magari matatu.

Mmoja wa wananchi waliobomolewa nyumba zao, Macarios Turuka  aliiambia JAMBO LEO kwamba eneo hilo kwa kipindi kirefu lilikuwa halitumiki na lilikuwa vichaka vya wahalifu ambapo wanawake walikuwa wakibakwa na kutumiwa na watu kwa uhalifu ndipo walipoingia na kujenga.

Aliongeza kuwa baada ya kuanza ujenzi, aliibuka mtu ajulikanaye kwa jina la Benjamin Mutagwaba akidai ni lake, ndipo walipofungua kesi Mahakama ya Kimara ambako alishindwa kupeleka vielelezo vya umiliki wa eneo hilo.

Mwanasheria anayetetea wananchi hao, Moses Chunga alisema kitendo cha kubomoa nyumba hizo ni ukiukaji sheria, kwani kuna kesi ya msingi namba 188/2016 waliyofungua Mahakama Kuu ya Ardhi ambapo walitakiwa Oktoba 31 waende kuisikiliza, lakini walishangaa kuona nyumba hizo zikibomolewa.

Alisema wananchi hao wanajipanga kudai fidia ya uharibifu huo na kuwa kabla ya yote wanahitaji kumwona Rais wapate haki yao.

Mkurugenzi wa Yono Auction Mart, Yono Kevela alisema kampuni yake imevunja nyumba hizo kwa amri ya Mahakama na polisi walikuwapo kusimamia.

"Mwenye eneo hilo ambaye ni Kanisa la Winers alishinda kesi mwaka mmoja uliopita na leo (jana) ulikuwa ni utekelezaji wa kuondoa wavamizi," alisema Kevela.

Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamisi alisema kitendo walichofanyiwa si cha kiungwana kwani wao wapo eneo hilo kwa 
siku nyingi hata kufikia hatua ya kujenga nyumba hizo,  mmiliki huyo alikuwa wapi kwa siku zote hizo.

"Kwa kweli hawa watu wanatufanya tusiipende Serikali yetu tunaomwomba Rais atusaidie katika jambo hili," alisema Hamisi.

Hamisi alisema leo wanatarajia kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kupeleka kilio chao na kama akishindwa watakwenda kwa Mkuu wa Mkoa na kama 
napo hawatapata ufumbuzi watakwenda kumwona Waziri William Lukuvi na Rais.

Hawa Musa alisema baada ya kuvunjiwa nyumba zao wapo katika wakati mgumu na hawajui wataishije na watoto wao.

Alisema wamepanga vitu vyao nje na mvua yote iliyonyesha jana ililowanisha vyombo vyao yakiwamo magodoro na hawajui huyo mtu anayedai ni eneo lake nyuma yake kuna nani.

"Tangu tufungue kesi Mahakama ya Kimara hakuwahi kufika, kama yupo kweli kwa nini anashindwa kuhudhuria mahakamani?" Alihoji Musa.

Musa aliongeza kuwa kabla ya kubomoa nyumba hizo walipaswa kutoa notisi, lakini hawakufanya hivyo walifika saa mbili asubuhi na kubomoa bila hata ya 
kushirikisha viongozi wa eneo hilo.

Mkazi mwingine, Juma Abdallah alilalamikia polisi kuchukua televisheni, kisimbuzi na Sh 80,000 ndani.

"TV yangu na kisimbuzi na Sh 80,000 zimechukuliwa," alilalamika Abdallah.

Katika hatua nyingine wananchi hao walimtupia lawama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tegeta A,  kuwa amekuwa akikumbatia watu wanaodai  kuwa eneo hilo ni lao, wakati anaelewa fika ukweli halisi.

Mwenyekiti huyo, Marko Vaginga alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kuzungumza chochote zaidi ya kumtaka mwandishi kwenda ofisini 
kwake.

"Nakuomba uje ofisini tuzungumze, kwa leo siko tayari kuzungumza chochote," alisema Vaginga na kukata simu.




Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo