Msichana kipanga la 7 kitaifa ataja siri ya ufaulu


Celina Mathew

MSICHANA pekee aliyeingia katika kumi bora ya wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, Justina Gerald, ameelezea siri ya mafanikio yake.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa simu jana, Justina aliyesoma shule tatu katika elimu yake ya msingi na kuhitimu katika Shule ya Msingi Tusiime, alisema moja ya siri ya mafanikio yake ni kujituma katika kujisomea.

Kwa mujibu wa Justina aliyesoma katika Shule ya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia la kwanza hadi la sita na baadae akahamishiwa Kaizirege, alikuwa akiamka saa 10 alfajiri kila siku na kujiandaa ambapo huanza kujisomea saa 12 mpaka saa moja asubuhi.

Baada ya hapo, Justina alisema saa moja huenda kunywa uji kabla ya kuanza ratiba ya kawaida ya vipindi vya darasani kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa tisa alasiri, ambapo hutoka kwaajili ya mapumziko ya jioni.

Justina alisema kuanzia saa 10 mpaka 12 hujisomea tena kabla ya kwenda kula chakula cha jioni, kisha saa moja usiku wanaingia darasani kwaajili ya vipindi vingine hadi saa mbili usiku.

Kuanzia saa mbili usiku, Justina alisema muda huo amekuwa akiutumia  kujisomea mwenyewe hadi saa tatu usiku ndipo huingia bwenini kwa ajili ya kulala.

Aliwashukuru waalimu wa Tusiime na kuwashauri wanafunzi wenzake kuwa na tabia ya kutokata tamaa kwa kuwa ipo siku watafanya vizuri na kujulikana kitaifa kama yeye kwani fursa zipo hivyo kinachotakiwa ni   kusoma kwa bidii.

Akisimulia alivyopata taarifa ya kufaulu kwake, Justina alisema  alipigiwa simu na baba yake na kuambiwa kwamba amepigiwa simu na walimu kuwa amefaulu vizuri na kumuahidi kuwa akirudi nyumbani jioni watazungumza.

Baada ya baba yake kurudi, alisema alimwita na kumpongeza na kumweleza kuwa atatafutwa na vyombo mbalimbali vya habari ili aelezea siri ya ufaulu wake hivyo atoe ushirikiano na pia mama yake alimpongeza.

Justina alisema ndoto yake ya baadae ni kuja kuwa mfanyabiashara maarufu au mhasibu na kilichomvutia ni mama yake na shangazi zake kufanya shughuli kama hizo.

Mwanafunzi huyo alisema akiwa nyumbani hupendelea kusoma vitabu vya hadithi kikiwemo cha 'Diary of the Wimpy Kid' na vinginevyo.

Alisema anapenda sana kusaidia watoto yatima na mara nyingi akiwa nyumbani hupendelea kumsaidia dada yake kuosha vyombo, kudeki, kufagia, kufua na kazi nyingine za nyumbani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo